UPENDO NKONE ACHUMBIWA
Ni miaka tisa (9) sasa ya ujane, lakini kwa Mungu hatukati tamaa, hatimaye mwimbaji wa muziki wa Injili Bongo, Upendo Nkone, amepata mwenza wa maisha ambaye ameanza na hatua ya mwanzo ya kumchumbia kabla ya kumbeba jumla, Risasi linabeba mabango ya nderemo.
Akistorisha na gazeti hili jijini Dar es Salaam juzikati, Upendo aliweka kweupe kwamba, amekuwa katika maombi ya mnyororo akimuomba Mungu ampe mume mwema ambaye atafanyika faraja katika maisha yake ikiwa ni pamoja na kupata heshima ya kuitwa mama fulani katika jamii inayomuzunguka.
“Namshukuru Mungu amejibu maombi yangu, tayari nimempata mwenza wa maisha ambaye ameanza hatua za mwanzo za kunichumbia, naye atafanyika faraja kubwa kwangu kwani nilidharaulika katika jamii inayonizunguka,” alisema Upendo kwa masikitiko makubwa.
Mtumishi huyo wa Mungu aliendelea kumwaga ‘data’ kwamba, kwa kipindi chote hiyo cha ujane amekumbana na misukosuko mingi ikiwa ni pamoja na kutokewa na wanaume wenye fedha zao ambao walionekana kuvutiwa naye, lakini Jehova alimuzuia na kuachana nao mpaka alimpompa wa kufanana naye.
“Nimeishi katika mazingira magumu ya ujane tangu mwaka 2002 nilipoondokewa na mzazi mwezangu, wanaume wengi walijitokeza wakitaka kunioa, moyo wangu haukuwa na amani nao licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha, ashukuriwe Mungu amenipa wa kufanana nami ambaye nitamuweka hadharani siku si nyingi,” alisema Upendo.
Aidha, staa huyo anayetesa na ngoma yake ya ‘Unitetee Mokozi Wangu’ alisema kwamba, suala la upweke, kukosa uhuru wakati wa usiku anapotoka kwenye huduma, ama kutembea usiku peke yake, kukaa na simanzi muda mwingi vimechangia kwa kiasi kikubwa kutulia katika magoti kumsihi Mungu ampe mbadala na mzazi mwenza.
Akielezea sababu za kutomuweka wazi kwa sasa mumewe mtarajiwa, Upendo alisema kuwa, anachoogopa ni wadaku ambao wanaweza kutibua na kumfanya aendelee kusota katika hali ya ujane.
Kondoo huyo wa Mungu alimalizia kwa kuwataka wajane wenzake kutulia katika uwepo wa Mungu ili wasiangukie katika dhambi ya uasherati kutokana na kuzungukwa na vishawishi vya kila namna, ambapo yeye binafsi alikuwa na mpango wa kuandaa tafrija fupi ya kujipongeza kuishi maisha matakatifu kwa muda wote huo.
Post a Comment