Askofu Kakobe akanusha kufanya maombi ya kuzuia umeme usiwake kanisani kwake
WAKATI Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) likiendelea na shughuli zake za kutandaza umeme wa KV 132 kutoka Ubungo hadi Makumbusho jijini Dar es Salaam, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Fellowship, Zachary Kakobe amelalamikia uzushi uliozushwa kuwa alisema kuwa umeme huo hautawaka utakapokamilika.
Akizungumza na mwandishi wetu juzi Jumapili Askofu Kakobe alisema waliozua uzushi huo wanashangaza kwa kuwa hakusema maneno hayo na kwamba kama wangekuwa wana uwezo huo basi waumini wa Kanisa analoliongoza wasingekuwa na sababu ya kukaa nje ya Kanisa usiku na mchana kulinda.
“ Ukweli ni kwamba watu wanavumisha kitu ambacho sikukisema, ni maneno ya kishetani, kama tungekuwa na uwezo wa kufanya umeme usiwake kulikuwa na sababu gani ya waumini kukesha hapa huku wakipigwa jua na mvua usiku na mchana?” alisema Askofu Kakobe.
Alipoulizwa anadhani kwanini watu hao wanamvumishia kitu ambacho hakukisema, kiongozi huyo wa kiroho alisema anachojua ni kwamba wavumishaji wana shetani mbaya na kwa watu kama hao dawa pekee ni kuwaombea tu waondokane naye.
“Watu wenye mapenzi mema na Kanisa wapuuze maneno hayo ambayo hata ukiyapima kwa akili ya kawaida utagundua kuwa yamezushwa na watu wenye maslahi nayo na kuwa na chuki na Kanisa,” alisema Askofu Kakobe.
Hivi karibuni Askofu huyo aliruhusu nyaya za Tanesco kupita nje ya Kanisa analoliongoza na baadhi ya vyombo vya habari vikaandika kuwa amesema umeme huo hautawaka utakapokamilika, hata hivyo, waandishi walioandika hawakufafanua maneno hayo aliyasemea wapi.
Post a Comment