Hakuna asiyeelewa Kwamba miaka ya hivi karibuni muziki wa injili umekuwa ukipanda chati kila kukicha, kutokana na kupata idadi kubwa ya wapenzi wa muziki huo ambao wamekuwa wakizifuatilia nyimbo za injili kwa makini pengine kuliko ile ya kidunia.
Nadhubutu kusema hivyo nikiwa na vigezo vya kutosha juu ya hilo na moja ya vigezo hivyo ni kufanya vizuri katika soko la muziki hapa nchini pamoja na nje ya nchi.
Leo hii ukipita katika maduka ya kuuza kanda, nyimbo ambazo utasikia zikipingwa ni zile za injili, hiyo ikiwa ni pamoja na wanunuaji wa kanda za jumla mara nyingi wamekuwa wanunua za muziki wa injili kuliko wa kidunia.
Lakini pamoja na mafanikio hayo ambayo kwa namna moja ama nyingine yameonekana kuwapatia ajira baadhi ya waimbaji wa muziki huo, bado kundi la Disciples linasema sanaa ya maigizo inalipa zaidi kuliko nyimbo za injili.
Kundi hilo linasema limekuwa katika sanaa ya maigizo kwa muda mrefu na limepata mafanikio kwa kiasi fulani, na siku za hivi karibuni limejiingiza katika harakati za kulihubiri neno la Mungu kwa njia ya uimbaji.
Akizungumza na safu hii kwa niaba ya wenzake, kiongozi wa kundi hilo Lazaro Philemon (Kibiwi), alisema pamoja na kwamba wapo katika sanaa ya maigizo, shauku yao ni kuhakikisha wanauona ufalme wa Mungu siku ya mwisho.
Alisema maigizo wanayoigiza yamelenga kulitanga jina la Mungu kwa njia hiyo na ndio maana wameamua kujitumbukiza tena katika fani ya muziki wa injili ili kupanua wigo wa mahubiri kwa njia ya sanaa.(DISCIPLES TEAM wakiwa katika picha ya pamoja)
Kiongozi huyo wa kundi la Disciples alisema sanaa ya maigizo waliianza mwaka 2003 kipindi hicho wakiwa shuleni, na tangu kipindi hicho wamekuwa wakitembea kila pembe ya nchi na nje ya nchi kwa lengo la kulihubiri neno la Mungu.
Mwaka 2008 mwanzoni kundi hilo limefanikiwa kurekodi albamu moja iliyopewa jina la Sadaka ikiwa na nyimbo nane.
Nyimbo zilizomo katika albamu hiyo ni, Kuna swali, Mbele yake, Aliteseka, Kilio, Vitani, Simama mwenyewe, Heri kuwa na Yesu na Sadaka ambao umebeba jina la albamu.
Wasanii wanaounda kundi hilo ni Philip Dilunga, Godfrey Lwiza, Mshana Chakupewa, Lazaro Philemon, Godfrey Sekumbo, Dions Bundara na Naomi.
Wasanii hao kwa pamoja waliiambia safu hii kwamba tangu waingie katika fani ya muziki wa injili, hawajapata faida kubwa ya kipato kama wanachokipata katika sanaa ya maigizo hali ambayo wanaona sanaa ya maigizo ni bora zaidi ya muziki wa injili.
Post a Comment