MWANSASU AJA NA WOSIA WA BABA
Hakuna asiyeelewa kwamba mkoa wa Mbeya ni mkoa ambao umekuwa ukitoa waimbaji mahiri wa muziki wa injili wenye tungo ambazo msikilizaji wa nyimbo hizo huwa hachoki kila anapozisikiliza.(Ephraim Mwasasu kulia akiimba kwa hisia kali)
Na kama wewe ni mpezi wa muziki huo naamini utaungana nami katika hili kwa sababu kila ukisikiliza nyimbo zenye mauzui mazito yanayowarejesha kwa Mungu watu waliopotea katika dimbwi la dhambi, ukiuliza ni nani kaimba wimbo huo, utasikia majina yanayoanza na Mwa…
Lakini wengi wameibuka miaka ya 2000 na kuliteka anga la muziki wa injili ndani na nje ya nchi. Miongoni mwa waimbaji hao ni Ambwene Mwasongwe, Bony Mwaitege, Ency Mwalukasa, Bahati Bukuku na wengine wengi.
Pamoja na majina hayo kuonekana kutesa katika anga hilo, lakini jina la Ephraim Mwasansu ni miongoni mwa majina ya waimbaji wa muziki wa injili nchini ambao hawachuji kila itwapo leo, na hiyo ni kutokana na umahiri wake wa kutunga nyimbo zenye mvuto na ujumbe mzito wa neno la Mungu na zisizochuja haraka.
Mwimbaji huyo ambaye huduma yake ya uimbaji ilianza tangu akiwa mtoto, alifanikiwa kurekodi albamu yake ya kwanza mwaka 1998 iliyojulikana kwa jina la Tutatesa milele ambayo ilionekana kuwashika watu wengi hali iliyomshawishi aingie tena studio mwaka 2001 na kufyatua albamu iliyojulikana kwa jina la Umepoteza namba.
Albamu hiyo nayo ilitikisa anga la muziki wa injili na kumpa moyo tena wa kuingia studio na kurekod albamu ya tatu aliyoipa jina la Msigombane ambayo bado inatesa katika anga la muziki ndani na nje ya nchi.
Hata hiyo Mwansasu ameamua kuifumua albamu yake ya pili inayojulikana kwa jina la Umepoteza namba baada ya kuonekana haina ubora wa kutosha na ametunga nyimbo nyingine tano ambazo zitakuwemo katika albamu ambayo ameipa jina la Wosia wa Baba.
Mwansasu ambaye sasa ni Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania lililopo Riverside jijini Dar es Salaam, alisema katika albamu hiyo atabakiza nyimbo tatu, ambazo ni Watoto wachanga, Umepoteza namba na Yumwema, ambapo nyimbo mpya ni pamoja na Wosia wa Baba unaobeba jina la albamu, Sitasahamu, Dunia ya sasa, Nakushukuru Mungu na Haleluya ulioimbwa kwa lugha ya kinyakwisa.
Safu hii ilitaka kujua ni kwa nini ameamua kuita Wosia wa Baba, Mwansasu alisema, kuna wosia ambao Mungu amempa kwa ajili ya kuwafikishia wanadamu ujumbe huo, ina inatarajia kukamilika mwezi April 2009.
Akielezea juu ya nyimbo zake kuendelea kuonekana kuwa ni mpya kila itwapo leo, Mwansasu alisema, siri kubwa ni kukaa katika unyenyekevu wa Mungu na kutobeza huduma za watu wengine.
Akielezea juu ya waimbaji wanaomkuna katika fani hiyo ya muziki wa injili, Mwansasu alisema anafurahishwa sana na huduma ya David Masaga Nyanda, David Robert na Fenuel Sedekia kutoka na miziki yao isiyoyumbishwa na kizazi cha sasa.
Mwansasu alisema kuwa si kwamba waimbaji wengine hawapendi isipokuwa hao aliowataja wanamvutia zaidi katika utunzi wa tungo zao nzuri na pamoja na staili yao ya uimbaji kuikubali wao wenyewe na nyimbo zao zikitoka huwa zinakubalika katika jamii.
Post a Comment