MCHUNGAJI JAMES MWAIPYANA
KUTOTII SAUTI YA MUNGU KUMEWAPONZA WAKRISTO WENGI.
Imeelezwa kuwa kitendo cha kutotii sauti ya Mungu kumewaponza wakristo wengi kuishi maisha ya dhiki kwa kuonewa na Ibilisi, nakujikuta wanalalamika kwamba Mungu hawasikii kila wanapomuita hali ambayo wengine hujikuta wanaachana na wokovu na kujitumbukiza katika imani za kishirikina.(Mchungaji James Mwaipyana Kulia akihubiri Neno la Mungu katika kanisa la Glory Temple Tabata)
Mchungaji James Mwaipyana wa kanisa la Glory Temple Tabata aliyasema hayo hivi karibubuni wakati wa mahubiri yaliyofanyika kanisani hapo na kuongeza kuwa kitendo cha wakristo kushindwa kuisikiliza sauti ya Mungu kunatokana na wahusika kushindwa kutofautisha kati ya sauti ya Mungu na sauti ya Ibilisi kutokana na kutopata elimu ya kutosha juu ya kuitambua sauti ya Mungu.
“ Wakristo wengi leo hii wamekuwa wakilia na matatizo wanayoyapata maishani mwao na wengine wamelazimika kuacha wokovu baada ya kuona wamefanya maombi kwa muda mrefu bila majibu na kudhani kwamba Mungu hawasikii, huku wakishindwa kutambua kuwa Mungu husema nao juu ya kilio chao bila wao kujitambua,” alisema Mwaipyana.
Mchungaji Mwaipyana alisema mbali na kutotii sauti ya Mungu, wakristo wengi wamekuwa na imani zenye mashaka ambazo kwa asilimia kubwa zimekuwa zikichelewesha miujiza yao na kuendelea kuishi maisha ya dhiki huku wakiwashuhudia wale wenye imani kali wakifanikiwa kwa kila wakiombacho kwa Mungu wao. (Mchungajia Mwaipyana kushoto akiwa na Mzee Kiongozi wa kanisa hilo Mzee Kapama wakiwa nje ya jengo la kanisa hilo)
Alisema hali hiyo ndio imewafanya wakristo wengi kuwa masikini kutokana na kitendo hicho cha kuwa na imani haba kwa kile wanachokiomba ikiwa ni pamoja na kushindwa kuisikiliza vema sauti ya Mungu ambayo hutoa maelekezo ya nini cha kufanya ili kujinasua na hali wanayopitia.
Aidha Mwaipyana alisema wakati mwingine Mungu hawaamusha watu usiku ili kuombea jambo ambalo liko mbele yao, lakini hujikuta wanashindwa kufanya hivyo kutokana na kuzidiwa na usingizi mzito, na jaribu kubwa linapowakuta hujikuta wanamnung’unikia kuwa kwanini anaruhusu hali kama hiyo.
“ Inasikitisha kuona kwamba Mungu hulazima kuwaamusha watu nyakati za usiku pindi anapoona kuna jambo la kuombea kabla halijatokea, lakini mhusika huamuka na kujikuta analala na kupatwa na usingizi mzito na jaribu linapompata anaanza kunung’unika kwamba kwanini Mungu ameruhusu hali hiyo,” alisema Mwaipyana.
Mchungaji huyo alisema kila itwapo leo Mungu huwa ana mbinu mpya kwa ajili ya watu wake ili kuhakikisha wanaishi maisha ya raha, lakini wahusika wamekuwa wakishindwa kufuata kila Mungu anachowaelekeza.
Post a Comment