CHRISTINA SHUSHO ANAYETESA NA UNIKUMBUKE
Kwa wapenzi wa muziki wa injili nchini, jina la Shusho si jina geni masikioni mwao kutokana na umahiri wa kutumia kipawa cha uimbaji cha mwanadada huyo anayetesa na albamu ya Unikumbeke ambayo imekuwa gumuzo kila vituo vya radio za dini hapa nchini pamoja na nje ya nchi.
Ukisikia nyimbo zake jinsi zilivyo na upako uliomo ndani ya nyimbo hizo unaweza kudhani kwamba mwana dada huyo huwa hawezi kuongea na watu kutokana na uimbaji wake wa nyimbo za taratibu na zenye mguso wa hali ya juu.
Ni ukweli usiofichika kwamba Shusho ghafla ametokea kukubalika katika jamii kutokana na nyimbo zake kuwagusa watu wengi na hiyo ikiwa ni pamoja na baadhi yao kupokea uponyaji baada ya kuchukua hatua kukiri kwamba Yesu ndio jibu la kila kitu.
Shusho pamoja na kwamba alifanikiwa kurekodi albamu yake ya kwanza iliyojulikana kwa jina la KITU GANI mwaka 1995, aliamua kujikita katika muziki huo mwaka 2004 na kuvuma na albamu hiyo ambayo nayo ilipata kibali katika radio zote za dini hapa nchini na nje ya nchi.
Hakuna asiyekubali kuwa Shusho hivi sasa ameliteka anga la muziki wa injili kukutokana na nyimbo zake kuchezwa mara kwa mara katika vituo vya redio hapa nchini. Kana kwamba hiyo haitoshi nyimbo za mwana dada huyo zinasikika kila kona ya nchini kwa wauzaji wa kanda kwenye maduka pamoja na mikokoteni.
Albamu yake ya pili ya ‘Unikumbuke’ imeonekana kuwagusa watu wengi kutokana na nyimbo zake kuwa na ujumbe mzito wa neno la Mungu na watu wengi wamemrudia Mungu wao baada ya kusikiliza nyimbo hizo.
Katika albamu hiyo kuna wimbo wa Unikumbuke, Bwana amenichagua, Mshukuruni Bwana, Adam, Wakuabudiwa, Hapo mwanza, Mtetezi na Tumsifu Bwana.
Hata hivyo katika nyimbo hizo nane nyimbo ambazo zimeonekana kuwakamata watu wengi ni wimbo wa Wakuabudiwa, Mtetezi na Unikumbuke ambazo zimekuwa zikisikika kila pembe ya nchi kwenye maduka ya kanda na mikokoteni pamoja na vituo vya radio za kidini.
Safu hii ilifanikiwa kukutana na mwanadada huyo ili kutaka kujua ni kwanini nyimbo zake zimetokea kupendwa na watu katika kipindi hiki na kuonesha dalili za kuwafunika waimbaji kama Bony Mwaitege, Bahati Bukuku na Rose Mhando kwa wauza kanda.
Yeye alisema, “Siri kubwa ya nyimbo zangu kupendwa na kila mtu ni kutokana na maombi ninayoyafanya kila siku na kisha kupata kibali kutoka kwa Mungu. Na si kweli nyimbo za waimbaji wenzangu zimefunikwa, lakini kila jambo lina wakati wake nadhani na mimi hiki ni kipindi changu na pia kwa msaada wa Mungu sitegemei kutoka katika ramani ya muziki wa injili kirahisi,.”Alisema Shusho.
Akizungumzia suala la uzinduzi wa albamu zake mbili, Shusho alisema maandalizi yote yamekamilika na tayari waimbaji mbalimbali wamethibitisha kushiriki katika uzinduzi huo ambao utakuwa ni wa tofauti ukilinganisha na zinduzi nyingine zilizowahi kufanyika hapa nchini.
Waimbaji watakaoshiriki katika tamasha hilo ni Bony Mwaitege, Bahati Bukuku, Upendo Nkone, David Robert, Rose Mhando, Ambwene Mwasongwe, Jackson Benti, Victor Aron, Miriam Lukindo, Papa Jonas Lutumba, Jojo Jose, na Debora John Said.
Watu wengi wanapojikita katika Fani ya uimbaji wa nyimbo za injili huwa hawajishughulishi na kazi zingine kutokana na sababu wanazozijua wao. Lakini kwa Shusho aliona suala la kufanya kazi nje na uimbaji ni muhimu sana ili kujikwamua kuchumi.
Mwana dada huyu mbali na kuwa mwimbaji wa muziki wa injili ni msanifu wa nguo mbalimbali na ana ofisi yake Kariakoo inayojulikana kwa jina la Ebenezer (Hata sasa Bwana ametusaidia) inayojishughulisha na upambaji wa maharusi, saluni za kike na kiume, ushonaji wa nguo na ufungaji wa vilemba.
Ili kudhihilisha kwamba yeye ana uhakika na anachokifanya, siku ya uzinduzi wa albamu zake ameandaa maonyesho ya mavazi ambayo ataonyesha siku hiyo.
Shusho amezaliwa katika familia ya wacha Mungu na ni mama wa watoto watatu ambao ni Odesia, Aim George na Hope. Kazi ya muziki wa injili aliianza mwaka 2004. Albamu yake ya kwanza aliitoa mwaka 1995 ambayo ndiyo ilimtambulisha rasmi katika anga la muziki.
One Response to “CHRISTINA SHUSHO ANAYETESA NA UNIKUMBUKE”
Bwana YESU asife,
Dada nyimbo zako zinanigusa sana ninapozisikiliza.
Mungu akubariki sana na azidi kukutumia kwa ajili ya ufalme na utukufu wake.
Songa mbele na zidi kumuomba MUNGU azidi kukupaka mafuta kwa ajili ya huduma hiyo.
Post a Comment