BONY MWAITEGE
Wengi wamekuwa wakimtazama katika sura mbili tofauti. Moja ni kijana, baadhi ya watu hawaamini kama anayoyaimba ndiyo anayoyatenda. Lakini hiyo haijalishi, kikubwa ni kuangalia matendo yake ambayo kwa macho pia yanaonekana.
Pili, ameoa juzi juzi. Utakatifu wake wa siku za nyuma alikuwa akiutunzaje?
Huyu si mwingine, ni mshika ‘maiki’ kuimba nyimbo za Injili nchini, Bonny Mwaitege.
Ameibukia kutoka wapi? Maana imekuwa ghafla tu mitaani ikaanza kusikika, Utantambuaje? Utantambuaje?
“Awali nilikuwa mcheza shoo kwenye kundi la Mchungaji Epharaim Mwansasu. Karibu kila wimbo wake katika Video mimi nimo kama mcheza shoo. Na nilikuwa ‘nikijituma’ hasa kwani napenda sana kucheza.
Je, alitoka kwa Mwansasu kwa sababu ya bifu au?
Mwaitege: Hapana! Hapana! Hakukuwa na bifu lolote lile. Mwansasu ni kama kaka yangu. Niliaga, akanipa baraka zote. Kwa sababu nilimwambia nataka kuimba mwenyewe. Na aliniahidi kunisaidia popote pale ambapo ningekwama. Ni kweli amekuwa akinisaidia sana.
Lakini namshukuru sana Mungu kwani toka nilipotoka kwa Mwansasu, ameniwezesha kuimba nyimbo zilizotokea kupendwa sana na wapendwa na hata wasiowapendwa.
Lakini nilipofika Dar kwa mara ya kwanza kabisa, nilipata ugumu kiasi cha kukata tamaa kabisa. Ilifika mahali nikajua sitaweza kuimba kama wengine. Mfano, dada Bahati Bukuku, dada Rose Muhando, mzee wangu Cosmas Chidumule na wengine wengi wenye majina yao. Pia nikaamini kama nitaweza kuimba, basi sitasimama kama wao. Lakini Mungu ni mkubwa sana, amenipa neema.
Ugumu aliokutana nao ni upi?
Mwaitege: Kwanza ni vigumu sana kuingiza kazi sokoni. Nina maana muingizaji mpaka akukubali, lazima uwe umemuomba sana Mungu.
Ukiongeza na ugeni niliokuwa nao, pia ulichangia nione ugumu.
Wengi wanasema kuwa, wimbo wa nangojea Mke Mwema ulikuwa maalum kwa ajili ya mke aliyemuoa katikati ya mwaka huu, kwamba baada ya kumchumbia ndiyo ukamtungia wimbo ule, kuna ukweli wowote?
Mwaitege: Inawezekana kuna ukweli. Lakini sikuutunga wimbo ule kwa ajili yeye alikuwepo. Ila naamini niliimba katika roho, na kweli nimepata mke mwema niliyekuwa namngojea. Anaitwa Subi Mwaitege.
Mara nyingi amekuwa akionekana yuko na mwimbaji mwingine maarufu wa nyimbo za Injili nchini, Bahati Bukuku. Je, ni ushirika wa kazi au kuna mengine yaliyojificha?
Mwaitege: Kusema ule ukweli Mungu anajua. Hata nikisema uongo anajua, nikiiba anajua, nikiwadanganya watu, yeye anajua, hakuna mtu alinisaidia sana nilipofika Dar es Salaam kama dada Bahati Bukuku.
Namchukulia kama dada yangu, kimuziki hata ushauri. Kuwa pamoja hadi leo niko naye pamoja, anakuja kwangu, ninakwenda kwake. Yeye amenionesha njia ya muziki wa Injili hapa Tanzania, ndiyo maana kwenye baadhi ya nyimbo zangu, kama Utantambuaje, sauti yake imo. Namheshimu sana dada Bahati.
Wimbo Utanitambuaje unaonekana ndiyo uliomuweka katika ramani ya muziki Mwaitege, lakini je, matendo yake yanafanana na wimbo wake huo?
Mwaitege: Nikisema matendo yangu na wimbo ule ni sawa sawa itakuwa kama najipalilia mwenyewe. Lakini naamini watu watakubali kwa kuniangalia matendo yangu.
Ana mikakati gani kwa siku za usoni?
Mwaitege: Ndoto zangu bado zipo. Siku moja nimiliki studio kubwa ya muziki wa Injili. Niwe na Meneja wangu, Mhasibu, wafanyakazi wengine mbalimbali ili kupeleka mbele kazi ya Bwana.
Post a Comment