The Best of David Robert iko sokoni
“ Miaka ya nyuma muziki wa injili ulidharaulika sana na mtu alipoonekana akiimba muziki huo alionekana kama kituko fulani hivi kwa sababu hakuna aliyekuwa anaguswa na nyimbo hizo.
Sio kwamba kipindi hicho hapakuwa na waimbaji wazuri wa muziki huo, la hasha! Walikuwepo tena wakali pengine kuliko waimbaji wa leo wanao mwimbia Mungu nyimbo za injili. Miaka hiyo kulikuwa na waimbaji kama Epharaem Mwansasu, Faustini Munishi, Mungu Four, Ency Mwalukasa, Jenifa Mgendi na miaka ya hivi karibuni alijitokeza Cosmas Chidumule aliyekuwa anapiga muziki wa dunia.
Na miaka hiyo ilikuwa ni mara moja sana kusikia muziki wa injili kukipingwa katika kumbi za starehe kama bar, kwenye harus nk. Lakini leo hii upepo umebadilika,”. Ndivyo alivyoanza kusema nami mwanamuziki mahiri wa muziki wa injili nchini David Robert aliyeibuka katika anga la muziki huo mwaka 2002 na albamu ya Baba.
Katika albamu hiyo Robert ambaye ana sauti nzito alishilikiana vema na Godwin Gondwe ambaye naye anasauti ya zege na kuifanya albamu hiyo kuwa na muvuto wa pekee na kuweka imara katika anga la muziki huo.
Albamu hiyo iliyokuwa ni nyimbo kumi iliwashika wengi na kila mmoja kupenda kuzisikiliza. Nyimbo zilikokuwa katika albamu hiyo ni Baba, Niongoze, Ngulujangu (kinyakyusa), Nakupenda, Hosana, Tufani, Mimi nani?, Bwana atafanya njia na We njoo.
Kufanya vizuri sokoni kwa albamu hiyo kulikuwa kama kumemtoa tongotongo machoni Robert. Kwani mwaka 2003 alilazimika tena kuingia studio na kufyatua albamu ya pili inayojulikana kwa jina la Kiganjani pa Mungu.
Albamu hiyo nayo imewakamata vema wapenzi wa muziki huo na kuanza kumtaka arekodi mkanda wa video ili iwe rahisi kwao kuwa wanamuona kwa njia hiyo japo wako naye mbali.
Albamu ya Kiganjani pa Mungu ilikuwa na nyimbo 8 ambao ni Neema, Sema nami, Shukurani, Nitakumbuka, E Yesu, Yesu ni Mungu na Kiganjani pa Mungu unaobeba albamu.
Hakuna asiyeelewa kila kitu kinachotengezwa kwa ubora, hutumia gharama kubwa kukikamilisha. Mwimbaji huyo alilitambua hilo baada ya kuona wapenzi wa muziki wake kumtaka arekodi hizo katika mtindo wa video.
Hata hivyo Robert alikaa na kutafari, kwa makini jinsi gani anaweza kurekodi video ambayo inaweza kuwa tofauti na video zilizotangulia. Jibu lake lilionekana kuwa ni kujiweka sawa katika fungu la fedha.
Robert aliamua kuzichambua nyimbo zilizo katika albamu hizo mbili na kufanikiwa kurekodi albau moja aliyoipa jina la The Best Of David Robert ambayo tayari iko sokoni kuanzia wiki iliyopita na inapatikana kwa njia ya HVS, DVD, na VCD.
Mwanamuziki huyo alisema kuwa albamu hiyo imerokodiwa katika madhari nzuri na mtaalam wa masuala ya filamu kutoka nchini Ujerumani Daniel Uphaus kwa kushirikiana na Sye ambaye ni mtaalamu wa kuongoza filamu.
Wataalu hao wameirekodi kwa makini albamu hiyo hali iliyopelekea kukubalika katika soko la kimataifa, ambapo tayari vituo vya Chanel O na Mtv Base wameiomba kwa ajili ya kuirusha katika runinga zao.
Ubora wa albamu hiyo ya The Best of David Robert umetokana na maandalizi ya miaka mitatu aliyoyafanya kabla ya kuchukua uamuzi wa kuingia studio na kutoa kitu hicho ambacho kinamvuto mkubwa.
Kukamilika kwa albamu hiyo kulichukua miezi minne na baada ya kurekodiwa aliipeleka kwa wataalam wengine kabla ya kuingia sokoni. Katika kuhakikisha albamu hiyo inakuwa tofauti na albamu nyingine hasa za muziki wa injili nchini, Robert alisafiri mikoa mbalimbali kwa ajili ya kupata picha nzuri kutokana na ujumbe wa nyimbo husika.
Mikoa aliyofanikiwa kwenda kurekodi albamu hiyo ni Morogoro, Iringa, Arusha, Moshi, Pwani na Dar es Salaam.
Aliyemvutia katika anga la muziki wa injili
Robert alisema kuwa huduma ya uimbaji alikuwa nayo tangu akiwa mtoto, ana alipokuwa shuleni huduma hiyo aliifanya kwa nguvu zote kwa kutembelea shule mbalimbali kwa lengo la kutoa injili ya njia ya nyimbo mwaka 1998 na kipindi hicho alikuwa akisoma shule ya sekondali Jitegemee ya jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kuipenda huduma hiyo, Mhungaji Elpham Mwansasu, Mchungaji Daniel Richard Mwansumbi na Cosmas Chidumule ndiyo waliompa hamasa kubwa Robert kujikita katika anga la muziki huo wa injili. Waimbaji hao ndio walikuwa wakimvutia kutokana na sauti zao kuwa nzuri pamoja na ujumbe wa nyimbo uliokuwemo ndani ya nyimbo hizo.
Mafanikio aliyoyapata kutoka na huduma ya uimbaji wa muziki huo
Kupitia muziki huo wa injili Robert amefaniki kujenga nyumba nzuri ya kisasa, ana gari nzuri. Mafaniko mengine alisema ni pamoja na kupata mtandao mzuri wa marafiki ndani na nje ya nchi na ana miradi mbalimbali inayomsaidia kuendesha maisha yake ya kila siku.
Matatizo anayokumbana nayo
Kuwa na mtaji mdogo wa kuitangaza huduma ya Mungu ndani na nje ya nchi, kutumia gharama kubwa katika kurekodi albamu na mwisho wa siku anajikuta mfukoni hana kitu.
Wito kwa wanamuziki wa injili hapa nchini
Anakerwa na waimbaji wanao kukimbilia katika muziki huyo kwa kuangalia pesa zaidi kuliko huduma. Ambapo watu wengi wamekuwa wakijikuta wanashindwa kufanya vema kazi ya Mungu pindi wanachokitarajia wanapokikosa.
Mwanamuziki anayemzimikia zaidi
Bila kificho David Robert alisema kuwa muimbaji mwenzake anayetamba na albamu ya Unikumbe Christina Shusho, ndiye anayemzimikia zaidi kutokana na nyimbo zake kuwa na ujumbe muzito ambao mara nyingi nyimbo hizo hugusa maisha anayopitia.
Matarajio yake ya baadaye
Ni kufanya mapinduzi makubwa katika muziki wa injili kwa siku za usoni. Mbali na hilo anatarajia kufanya uzinduzi wa albamu hiyo mwishoni mwa mwaka ujao. Je unamaoni gani kuhusu huduma ya David Robert? Usisite kunitumia maoni yako.
Post a Comment