Uchaguzi 2010: Maaskofu watoa ujumbe mzito
MALASUSA ADAI VIONGOZI WANG’ANG’ANIZI WATABAINIKA
HOMA ya uchaguzi mkuu mwakani imeanza kupanda miongoni mwa viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali ambao wametumia mahubiri yao katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi kuwaonya wanasiasa na kutahadharisha wananchi kuwa waangalifu wakati taifa linajiandaa na uchaguzi huo.
Akitoa mahubiri katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam jana, Akofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa alisema dhana ya kung’ang’ania madaraka itajidhihirisha mwakani wakati wa uchaguzi mkuu.
Alisema katika kipindi hicho wabunge hujitokeza na kuonyesha kwamba wao ndiyo wamiliki wa majimbo.
“Ving’ang’anizi tutawaona mwakani katika uchaguzi mkuu, mara watajitokeza wabunge watakaosema hili ni jimbo langu…hivi ndivyo Herode alivyokuwa baada ya kusikia Yesu amezaliwa na atakuwa mfalme,” alisema.
Dk. Malasusa alibainisha kwamba si wabunge pekee wenye hulka hiyo bali hata maofisini tabia hiyo bado ipo.
Kwa upande mwingine, alieleza dunia ya sasa imejaa ukandamizaji na pia haimjali mtu masikini na kuwataka waumini hao kupendana.
Aliwasifu wazee kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhudhuria ibada na kuwataka kuwahamasisha vijana nao kufanya hivyo kwani kwa sasa hali yao kiimani inazidi kuwa mbaya.
Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki, Dar es Salaam, Methodius Kilaini, aliwataka viongozi wa vyama vya siasa na Watanzania kuwa waangalifu wakati taifa linajiandaa na uchaguzi mkuu, ili kuepuka vurumai kama mataifa mengine.
“Leo tunaposherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo, napenda kuwakumbusha kuwa mwaka 2010 ni mwaka wa uchaguzi mkuu… hiki ni kitu muhimu mno, tunaomba ufanyike kwa amani na kwa mafanikio makubwa, ili kuepuka matatizo.
“Nawaomba viongozi wa vyama vya siasa, wapitishe zoezi hili kwa usalama, upendo ili mwishowe tufike mwisho wa siku tukiwa salama,” alisema.
Askofu Kilani ambaye sasa amehamishiwa katika Jimbo Kuu la Bukoba, alisema kutokana na mapenzi aliyonayo Mungu kwa taifa hili, Watanzania wanapaswa kuendeleza upendo, mshikamano na uelewano uliopo.
“Tuombe msamaha pale tulipokosea, Mungu awape nguvu, umoja na uelewano miongoni mwenu ili kudhihirisha kweli leo tunaadhimisha mtoto, mkombozi Yesu Kristo amezaliwa ili kutukomboa,” alisema.
Aliwasihi waumini kote nchini kuendelea kuliombea taifa kwa yote yaliyotendeka ingawa hakufafanua ni mambo gani.
Katika hatua nyingine, Askofu Kilaini alitumia nafasi hiyo kuwaaga rasmi waumini wa dhehebu lake mkoani Dar es Salaam, huku akisisitiza kuwa atawakumbuka kwa ukarimu wao ambao amekuwa nao katika utumishi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
“Narudishwa kwenye jimbo ambalo nimetoka miaka 37 iliyopita, napenda kuwahakikishia kwamba nitaendelea na uzi uleule wa kutetea kile ninachokiamini,” alisema Askofu Kilaini.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Valentino Mokiwa aliwataka viongozi wa serikali kuzaliwa upya ili kuepuka matatizo yanayowapata.
Aliyasema hayo juzi usiku wakati wa mkesha wa Sikukuu ya Krismasi kwenye Kanisa la St. Albano, Dar es Salaam ambapo alisema kutokana na matukio yanayowapata viongozi wanastahili kuzaliwa upya ili kuepuka aibu kwa taifa.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Kardinal Polycarp Pengo aliwatoa hofu waamini wa dhehebu juu ya uchaguzi mkuu ujao kuwa utakuwa wa haki na amani.
Askofu Augostine Ndeliakyama Shao wa Kanisa la Minara Miwili, Mji Mkongwe, Zanzibar, alisema viongozi wa siasa nchini wanakwepa kuwapa wananchi elimu ya uraia, kwa kuhofia watawakataa katika uchaguzi baada ya kuelewa haki zao za msingi.
Akizungumza wakati wa ibada ya mkesha wa Krismasi, alisema: “Elimu ya uraia inapingwa na baadhi ya wanasiasa, kwani wanajua elimu ni nguvu ya mnyonge, hivyo hawatapata fursa ya kudanganya wapiga kura.”
Askofu huyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea misingi ya haki za binadamu na utawala bora nchini, alisema hivi sasa taifa linakabiliwa na tatizo la kukithiri kwa ufisadi na kuathiri wananchi wanyonge na kunufaisha wawekezaji kutoka nchi za kigeni.
Alisema kilio cha Watanzania wengi hivi sasa ni kukithiri kwa ufisadi na kwamba njia pekee ya kuondokana na hali hiyo ni kufanyika mabadiliko ya kiuongozi.
“Umasikini uliokithiri katika jamii ni wimbo usiofurahisha kwa rushwa na ufisadi, wizi wa mali ya umma na kutowajibika kwa viongozi wa jamii, haya yote ni madhaifu yanayoashiria tupo gizani na kuna ulazimika wa mabadiliko,” alisema.
Alisema Tanzania hivi sasa ni nchi ya 102 katika orodha ya nchi 180 zinazotajwa kukithiri kwa rushwa, na itaendelea kukamata nafasi hiyo mbaya, iwapo suala hilo halitapigwa vita katika uchaguzi wa mwakani.
Aidha, alisema kitendo cha wafanyabiashara Zanzibar kuachiwa kupandisha bei ya mafuta ya dizeli wapendavyo, ni kielelezo kwamba wahusika wa kulinda sheria za nchi hawawajibiki na hivyo kusababisha athari kubwa kwa wananchi.
Alieleza viongozi wote wana wajibu wa kusimamia haki na maslahi ya raia na hivyo haikuwa haki kuachiwa kupandisha bei za mafuta watakavyo.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdernbug Mdegella, aliwataka Watanzania kuepuka kuendelea kulalamika dhidi ya mawaziri na wabunge mafisadi, kwani hawakujiweka madarakani bali wamewekwa na wananchi na kwamba dawa ya kuwaondoa mwakani ipo mikononi mwao na si mahakama.
“Watanzania hatujui kuchagua viongozi bora na ndiyo maana tumekuwa watu wa kuwalalamikia viongozi mafisadi wakati chungu cha kupika mafisadi ni kura zetu,” alisema.
Alisema wabunge na mawaziri wanaolalamikiwa kwa ufisadi na uwajibikaji mbovu katika nafasi zao wamefika bungeni na kuteuliwa mawaziri baada ya wananchi kuwapigia kura na kusema kwamba kama wanaamini walifanya makosa katika uchaguzi huo wasirudie tena makosa hayo kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
Akitoa salamu baada ya kumaliza shughuli za ibada ya tatu katika Usharika wa Iringa Mjini, alisema kwa upande wake ameamua kwa mwakani kuzungumzia mambo makuu manne likiwemo la wakazi wa Iringa kutoogopa kufa hata kuamua kujinyonga, suala la kilimo ambalo wananchi wanauelewa mkubwa ila wanakwamishwa na viogozi wabovu, ushuhuda wa kikristo kwa kuepuka kufanya maovu wakati wa sikukuu na kupata viongozi bora.
Hivyo hivyo, alisema ili kumpata kiongozi bora ni lazima kila Mtanzania mwenye sifa kujiandikisha kupiga kura na kushiriki kupiga kura wakati wa uchaguzi.
Aidha, alisema Watanzania wamekuwa ni watu wa kulalamika kuhusu viongozi mafisadi huku wao wakikwepa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Hivyo alishauri kuwepo kwa mkakati kamili kutoka kwa wananchi wote ili kuhakikisha wale wenye sifa wanajitokeza kugombea nafasi mbalimbali bila kujali chama cha siasa kama njia ya kuwaondoa viongozi mafisadi.
“Nimewaambia Iringa haiendelei kwa sasa, tunashindwa kuchagua viongozi bora… sasa ili kupata viongozi bora lazima wote tushiriki kuchagua viongozi pamoja na kujitokeza kugombea kwa wale wenye sifa… wengine wanasema tatizo viongozi waliochaguliwa ni mafisadi tu… sasa wewe usiye fisadi mbona hujagombea?” alihoji.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, aliitaka jamii kuiombea nchi katika uchaguzi mkuu ujao kwani mazingira yaliyopo yanaonyesha kukosekana kwa haki na amani na kuongeza kuwa kanisa hilo litaandaa semina mbalimbali za kuelimisha wanajamii kuhusu haki zao kama kupiga kura.
Habari hii imeandaliwa na Kulwa Karedia na Sauli Giliard (Dar), Makame Amer (Zanzibar), Francis Godwin (Iringa) na Beatrice Maina kutoka Moshi.
Chanzo:tzdaima
Post a Comment