Uhohe hahe wa wasanii umewatajirisha Wadosi
Ni ukweli usiofichika kwamba waimbaji wetu wa muziki wa injili pamoja na wa mataifa wengi wamekuwa wakiishi maisha duni kutokana na kushindwa kufaidika na kazi zao pindi zinapoingia sokoni. Waimbaji hao wamekuwa wakitumia gharama kubwa katika kuiandaa albamu kwa malengo kuwa, siku moja pesa yake hiyo itarudi kutokana na mauzo ya kanda, CD, ama DVD, VCD na VHS.
Kabula naye ni miongoni mwa waimbaji wa muziki wa Injili wanaolia na tatizo la dhuruma kutoka kwa wasambazji wa kazi za wasanii mbalimbali hapa nchini. Mwimbaji huyo ambaye tayari amekamilisha albamu yake ya pili inayokwenda kwa jina la Ushindi alisema kuwa, tatizo la uhohe hahe wa wasanii wetu ndiyo kimekuwa kigezo kwa wasambazaji wenye asili ya Kihindi ‘Wadosi’ kujitajirisha kupitia kazi za waimbaji hao.
Kabula alisema kuwa, wadosi hao wamebaini udhaifu wa waimbaji wa fani mbali mbali na kuona ni wakati mwafaka wa kujipatia kipato cha kuendeleza maisha yao bila kutoa jasho lolote na kuwaacha wahusika wakiishi maisha ya dhiki.
Muimbaji huyo alisema kuwa, wasambazaji hao wamekuwa wakiwaibia watumishi wa Mungu na wasanii kwa kutoa kopi nyingi wakati wa kudurufu ikiwa ni pamoja na kuwapa pesa ndogo mara baada ya kuingia nao mikataba.
“ Inasikitisha sana kuona jasho letu linaliwa na watu wachache ambao wamebeba jukumu la kusambaza kazi zetu, na hii inatokana na uhohe hahe walionao waimbaji wengi. Muimbaji hutumia gharama ya kurekodi, kwa sababu mpaka kukamilika kwa kazi hiyo, kunaweza kugharimu kiasi cha shilingi laki nane, hivyo pesa nyingi inatumika katika shughuli hiyo tu, na pindi kazi inapokamilika utakuta muimbaji hana fedha hata kidogo,” alisema Kabula.
Alisema, ni ukweli usiopingika kuwa, waimbaji hasa wa muziki wa Injili endapo wangekuwa na mitaji ya kutosha ya kuwawezesha kusambaza wenyewe kazi zao, leo hii hakuna msanii ambaye angekuwa analia na kunyonywa na wadosi, kwa sababu wao ndiyo wangekuwa wamiliki wa shughuli zote.
Kabula alitoa mfano kwa nchi kama Kenya ambapo baadhi ya watumishi wa Mungu na wasanii kazi zao wanasambaza wenyewe, hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kujikwamua kiuchumi kutokana na kipato wanachokipata baada ya kuuza kazi zao. Alisema kuwa, leo hii wadosi hao wanapanga pesa ya kumpa muimbaji husika. Mpaka leo hii kuna waimbaji wanapewa shilingi mia 100 kwa kopi moja na wengine 200 na 300.
Kabula aliongeza kuwa, tangu miaka ya 90 kipindi ambapo kanda moja ilikuwa inauzwa shilingi 700, msanii alikuwa analipwa 100 au 200 kwa kopi moja, na leo hii kanda moja inauzwa 1500 lakini muimbaji bado analipwa kiwango hicho cha pesa kwa kopi moja.
Akizungumzia suala la wezi wa kazi za waimbaji wa muziki wa dini na wa mataifa, Kabula alisema, huko nako kunatatizo kubwa sana na hiyo inamfanya muimbaji wa asiwe na namna yoyote ya kula vema matunda ya jasho lake.
Alisema kuwa, licha ya kuwepo kwa chama cha Kutetea Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ambacho kina jukumu la kusimamia na kulinda kazi za wasanii hapa nchini, kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Bunge mwaka 1999, bado tatizo la kuibiwa kazi zao lipo na linaendelea kwa kasi kubwa.Wizi huo umeshamili vilivyo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na mikoa mingine iliyompakani mwa nchi za
Alisema kuwa hali hiyo inatokana na kutokuwa na sheria za kulinda na kutetea vema kazi za wasanii hapa nchini. Kwa mfano miaka ya hivi karibuni, COSOTA ilifanikiwa kukikamata kiwanda cha kuzalisha nyimbo za wasanii mbalimbali eneo la Buguruni Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, lakini cha kushangaza mtuhumiwa huyo alilipa faini ya 200,000 tu ambayo hailingani na gharama ambazo wamiliki wa kazi hizo waligharamia katika kuzitengeneza.
Aidha, hivi karibuni, Chama cha Haki Miliki na Shiriki Tanzania , COSOTA, ambacho kinasimamia kazi za wasanii, kiliwanasa watu wawili waliokuwa wanajihusisha na shughuli ya kudurufu kazi za wasanii zenye thamani ya sh.161milioni .
Watu hao ni Loveness Masonda, wa Tabata na Ayaj Chavda , wa Kariakoo, ambao kila mmoja kwa wakati wake walitengeneza na kuuza kazi hizo bila vibali vya wamiliki wa kazi hizo.
Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani, lakini mpaka sasa haijulikani nini kinaendelea juu yao . Afisa Mtendaji Mkuu wa Cosota, wa chama hicho Yustus Mkinga alisema kuwa, Loveness alikuwa anamiliki mtambo wa kudurufu wenye uwezo wa kufyatua kaseti 16 kwa dakika tatu, nyumbani kwake na alikuwa na karatasi maalum pamoja na vyombo vya kudurufia 'scanner' anavyotumia kuiba kazi za wasanii na kubandika nembo ambayo si rahisi kwa mteja kugundua kuwa ni feki.
Ilielezwa kuwa, Shavda alikuwa akitengeneza kwa kununua nakala moja ya picha za kihindi na kubadili lugha ya picha hiyo kuwa kwa kiswahili na yeye kutengeneza kopi zaidi ya laki tatu na kuziuza mitaani huku zikitoka kwa nembo yake kama mmiliki halali wa kazi hizo.
Post a Comment