Mtikila arudishwa rumande
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana (Jumatatu) ilimfutia dhamana Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila na kumrudisha rumande baada ya mwanasiasa huyo kukiuka masharti ya dhamana yake.
Mtikila anayekabiliwa na tuhuma za kumwita Rais Jakaya Kikwete gaidi, alitiwa nguvuni na polisi baada ya Hakimu Mkazi Elirehema Lema kudai mchungaji huyo kushindwa kufika mahakamani hapo kwa muda muafaka.
Kwa mujibu wa hakimu huyo,ni mara ya pili sasa Mtikila kuchelewa mahakamani hapo bila kutoa taarifa zozote kwa wadhamini wake kama masharti ya dhamana yanavyoelekeza.
Hata hivyo, Mtikila alidai mahakamani kuwa, alikuwa anaumwa na kuongeza kwamba, taarifa za kuumwa kwake alimpatia Wakili wake ambaye naye alidai mwanawe anaumwa na hivyo mahakama kushindwa kupata taarifa zake.
“Ni mara ya pili sasa umekuwa ukirudia kosa hili bila kutoa taarifa zozote kwa wadhamini wako hivyo ninakufutia dhamana utarudi rumande hadi Januari 25, mwaka huu kesi yako itakapoletwa kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya awali,” alihitimisha Hakimu Lema.
Januari 4, mwaka jana, mtuhumiwa hakufika mahakamani hapo ambapo upande wa mashitaka uliiomba mahakama hiyo kutoa kibali cha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kutokana na kutofika kusikiliza kesi inayomkabili bila kutoa taarifa yoyote wala maombi ya kumfanya ashindwe kufika mahakamani.
Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Victoria Nongwa hakutoa kibali cha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo licha ya kuombwa na upande wa mashitaka.
Januari 6, mwaka jana, Mtikila aliwasilisha barua ya kuiomba msamaha mahakama hiyo, akieleza kuwa alikuwa akimhangaikia ndugu yake ambaye amepooza na kudai kuwa aliwatuma wadhamini wake kutoa taarifa hiyo lakini hawakufanya hivyo.
Inadaiwa kuwa,Oktoba 21, 2007, maeneo ya Ilala katika Shirika la Nyumba (NHC) la Taifa, Mtikila alitoa maneno ya dharau na kujenga chuki dhidi ya Serikali ya Rais Kikwete.
Katika shitaka la pili, Mtikila anadaiwa kutoa lugha ya uchochezi akidai: “Ahadi zote za Rais Jakaya Kikwete siku zote zinaongozwa na imani yake ya dini tena kutekeleza malengo yake ya kusilimisha nchi”
Mtikila alikana mashitaka hayo na alikuwa nje kwa dhamana.
Post a Comment