MIRIAM LUKINDO: Majungu, chuki na fitna vitaua muziki wa Injili
Leo katika safu hii tunaye mwimbaji mkongwe wa nyimbo za Injili Tanzania, Miriam Lukindo.
Licha ya kudumu kwa muda mrefu katika muziki wa injili, jina lake si kubwa kama ilivyo kwa wanamuziki kadhaa wa miaka ya hivi karibuni.
Miriam ambaye alianza fani hiyo tangu mwaka 1997, anasema muziki wa Injili umekua kadri siku zinavyokwenda kutokana na wengi wao kuelewa neno la Mungu na kuacha tabia za kidunia, licha ya kusisitiza kuwa kuna baadhi ya wanamuziki wachache ambao wamekuwa wakitumia muziki huo kwa ajili ya kujineemesha na kutozingatia mafunzo ya kimungu.
Ameeleza kuwa wanamuziki hao wenye tabia ambazo siyo nzuri nyuma ya pazia, wamekuwa wakitumia kila njia kuhakikisha wanapata umaarufu pasipo kuzingatia maadili ya muziki huo na mafunzo yake.
“Katika miaka ya nyuma waimbaji walikuwa wakiiimba kwa ajili ya kumsifu Mungu na kuonyesha vipaji vyao vya kweli, tofauti na sasa watu hufanya kama biashara na sehemu ya kupatia umaarufu kitu ambacho ni chukizo mbele za Mungu,” anasema Miriam na kuongeza kuwa.
“Kutokana na hali hii wanamuziki wengi wamekuwa wakiishia njiani kwa sababu wanakosa mwendelezo wa kile wanachokianzisha huku wakiwa hawana malengo endelevu ya kiungu. Waimbaji wa aina hiyo wamekuwa wakisababisha muziki wetu kuyumba na kuonekana haufai.”
Alishauri kuwa ili muziki anaoimba upate maendeleo, ni vema kukawa na ushirikiano baina ya wasanii wenyewe ili kuhakikisha wanaandaa kazi zao pamoja, kushirikiana na kuomba ushauri pindi kati yao anapotatizwa na jambo.
Akitolea mfano kwa wanamuziki chipukizi ambao wengi wao hawapendi kuomba ushauri na matokeo yake kujikuta wakifanya kazi kubwa isiyo na faida wakati hali hiyo ingeweza kuzuilika.
Alieleza kuwa wizi wa kazi za wasanii nao umekuwa tatizo katika kushuka kwa soko lao. “Wengi wetu hatujui sheria na pia hakuna sheria inayowabana wauzaji wa kazi zetu wanaofanya hivyo kinyume cha sheria.
“Tatizo lingine ni kutokuwa na uongozi mzuri kwa baadhi ya waimbaji wanaoongozwa kutokana na wengi wao kutokuwa waaaminifu ndiyo maana hatufaidiki zaidi ya kuishia kujulikana,” anasisitiza Miriam.
Mwimbaji huyu kwa sasa amekamilisha albamu mbili, ya kwanza ilijulikana kwa jina la ‘Sote Na Tuimbe’ aliyoitengeneza Nairobi, Kenya na ya pili ni ‘Asubuhi’ aliyoirekodia Arusha na Dar es Salaam. Kwa sasa yupo studio akipika albamu ya tatu itakayojulikana kwa jina la ‘Double Double’.
Nje na muziki ni mama wa familia ya mtoto mmoja akiwa na mipango ya kuwa na watoto wengine zaidi katika siku zijazo, ana mipango kadhaa kwa ajili ya kufungua miradi yake binafsi itakayomwongezea kipato nje na uimbaji.
Ameshauri wanamuziki kuacha kuchukiana miongoni mwao, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wakienda kinyume na kile wanachokiimba na kusababisha kushuka kwa thamani ya muziki huo.
Post a Comment