MZEE WA UPAKO
Mzee wa Upako, Mchungaji Anthony Lusekelo (pichani) amemtibulia kupata wateja Mchungaji Ambilikile Masapile baada ya kuweka kambi katika Jiji la Arusha ambako aliibuka akiwa na maji na mafuta ya upako.
Baadhi ya wagonjwa waliozungumza na mtandao huu akiwemo Suzan John, walisema kwa nyakati tofauti kuwa, waliambiwa kwamba Mzee wa Upako yupo jijini hapo, na kwa kushawishiwa na baadhi ya wagonjwa waliokwenda kwa Babu na kutopata nafuu waende kwa Mzee wa Upako kuliko kuendelea kungoja foleni ya kwenda Samunge.
“Mimi kuna mtu aliniambia matatizo yangu yanaponywa na Mzee wa Upako, hivyo nikaamua kukatiza safari ya Samunge nikaenda Metropole Sinema na kweli nilipoombewa tatizo langu likatoweka,” alisema Suzana aliyedai kutoka Bunda.
Mwandishi wetu alishuhudia wagonjwa wengi kutoka mikoani wakiacha safari ya kwenda kwa Babu na kuhudhuria maombi ya Mzee wa Upako ambaye alitangaza wazi kuwa, kwake kuna uponyaji wa kweli wa Mungu.
Akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu, Mchungaji Lusekelo alikiri kuwa ni kweli aliweka kambi Arusha na kuokoa watu wengi ambao walitaka kwenda kwa Babu na hata wale waliokwenda na kutoponywa.
“Kwanza siku hiyo kulikuwa na mvua nyingi sana, nikaikemea na ikaacha kunyesha, upinde wa mvua ukakunjika katikati ya uwanja, watu walishangaa sana.“Lakini pia kulikuwa na wagonjwa, kwa mfano mama mmoja alikuwa mjamzito na alikuwa hajifungui, kuna mzee mmoja alikuwa amevimba miguu na baadhi yao walipata kikombe lakini hawakupona, niliwaombea na wakapona,” alisema Mzee wa Upako.
Alipoulizwa njia anayotumia kuponya watu alisema:”Ninatoa maji ya uzima ambayo nayabariki kwa mikono yangu na yanatibu magonjwa sugu tofauti na hicho kikombe kimoja wananchi wanachokikimbilia huko Loliondo,” alisema Lusekelo.
Akaongeza kuwa, anaamini maji hayo anayotoa ni zaidi ya kikombe cha Babu wa Loliondo na amewaomba wananchi kuyanywa kwani yanaponya magonjwa sugu.
Alitamba kuwa, alilitikisa anga la Mkoa wa Arusha baada ya kupata mapokezi makubwa licha ya kuwepo kikombe cha Babu huyo.
One Response to “MZEE WA UPAKO”
kiongozi tunakuamini
Post a Comment