KABULA AWASHANGAZA WATU KWENYE MUZIKI WA INJILI
Mwimbaji wa muziki wa Injili nchini anayechipukia kwa kasi kubwa katika fani hiyo Kabula J.George amewaduwaza waumini wa Huduma ya Neno la Upatanisho iliyopo Kivule nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam baada ya kuimba nyimbo tatu mfululizo na kupelekea nguvu ya Mungu kushuka mahali hapo na kujikuta watu wote wakizama katika maombi na kusimamisha taratibu zote za ibada kama ilivyozoeleka.
Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita wakati Kabula akiitambulisha albamu yake mpya aliyoipa jina la Ushindi ndipo akasimama kuimba nyimbo hizo huku waumini waliokuwa wamejazana katika huduma hiyo wakifuatilia kwa makini ujumbe uliokuwa ndani ya kila wimbo na alipoimba wimbo wa Dhihilisha, taratibu kila mmoja alianza kububujikwa na machozi mazito na kuzama kwenye maombi.
“ Tungu nianze kufanya huduma katika Huduma hii ya Neno la Upatanisho, sijawahi kuona mwimbaji mwenye nyimbo zenye mguso wa ajabu kama za Kabula, hakika kila mmoja wetu amejikuta akibubujikwa na machozi na kisha kuzama kwenye maombi kutokana na ujumbe mzito ulio ndani ya nyimbo hizo, nililazimika kusitisha taratibu zote za ibada na kuanza kutoa huduma ya maombezi,” alisema Mchungaji wa Huduma hiyo Nicolaus Suguye.
Albamu ya Kabula George imeonekana kukubalika kwa wapenzi wa muziki wa Injili nchini, kutokana na nyimbo zake kuwa na ujumbe mzito ambao kila mmoja amekuwa akiguswa nao, na wengi wamezikubali kutokana na vionjo vya maneno ya Mungu aliyoyatumia.
Post a Comment