MWIHAVA: HUDUMA KWANZA, ‘SHEKELI’ BAADAYE
WAIMBAJI wa muziki wa injili wamekuwa wakiongezeka kila iitwapo leo, na baadhi yao huangalia fedha kwanza badala ya huduma waliyoitwa na Muumba wao.
Kama unafikiri nakudanganya fanya uchunguzi wa kina uone, ni waimbaji gani walioibuka kwa kasi ya ajabu katika muziki huo wakidhani kwamba watapata mafanikio ya haraka, na mipango yao ilipogoma walilazimika kuanza biashara nyingine.
Haitakuwa busara kuwataja watu hao kwa majina, lakini wengi nawafahamu na leo hii huwa nikikutana nao mitaani, nawaona wamerudi hatua kumi nyuma katika masuala ya kiroho.
Baadhi yao pia wanapofanikiwa kukamilisha albamu zao, hukimbilia kuandaa matamasha kwa kivuli cha kuchangisha fedha zitakazowasaidia watoto yatima na wajane ama chochote watakachoona kinafaa kuwashawishi watu wengi wahudhurie katika shughuli hiyo.
Nyuma ya pazia huwa wanafahamu kwamba, baada ya kukusanya fedha hizo wataenda kuzifanyia nini pesa kwa sababu hakuna mtu atakayeuliza kwanini wanafanya hivyo.
Kama nilivyosema hapo awali kwamba ni baadhi ya waimbaji wana tabia hiyo, lakini wengine wanapoingia katika suala la uimbaji huwa hawaangalii fedha kwanza bali huduma kisha pesa baadaye.
Miongoni mwa watumishi wa Mungu ambao kwao suala la pesa haliko mbele sana ni Daniel Mwihava mwimbaji kutoka mkoa wa Iringa anayefundisha kwaya ya kanisa la House Grace lililopo Kimara Bucha jijini Dar es Salaam.
Mwihava anasema: “Binafsi moyoni huwa najisikia kuhukumiwa kuanza kuomba fedha kwanza kabla ya kufanya huduma. Mara nyingi huwa nafanya huduma kwanza, ‘shekeli’ baadaye.
“Katika huduma hii ya uimbaji, unapomtumikia Mungu katika roho na kweli, fedha zitakuja zenyewe kwa watu kutoa kwa hiyari yao bila kusukumwa, kwa sababau upako wa Jehova unakuwa juu yako hivyo kila mmoja kutaka kukuita kwenye semina, mikutano, makongamano, harusi na shughuli nyinginezo”.
Mwihava anatarajia kukamilisha albamu yake ya kwanza mwishoni mwa mwezi huu aliyoipa jina la Kumbuka kushukuru ikiwa na vibao vinane kama, Tokeni, Safari ya mbinguni, Mwinatilege(Kihehe), Msiipende dunia, Usihofu maisha, Msahama, Twinoma (Kihehe) na Kumbuka kushukuru.
Alianza kufundisha kwaya ya Uamsho iliyopo kijiji cha Wami wilayani Mfindi mkoani Iringa mwaka 1995. Mwaka 2000 alijiunga na kwaya ya Bethel kabla ya mwaka 2008 kwenda kuifundisha kwaya ya Victor zote za EAGT Iringa.
Mwihava alimaliza kwa kuwataka waimbaji wa muziki wa injili nchini kumtanguliza Mungu kwa kila jambo wanalolifanya ili kujihakikishia huduma na kukubalika katika jamii.
Post a Comment