Rosemary Nyato alia na Studio
Lakini maono ya watu hao yamekuwa yakikwamishwa na wajanja wachache ambao wamekuwa wakiendesha maisha yao kwa kupitia mgongo wa wasanii hao.
Katika hali ya kusikitisha kumbe wasanii hawa, wanapati matatizo kwa wasambazaji peke yao, eneo lingine ambalo watu hawa wamekuwa wakitabika ni studio. Eneo hili kwa kiasi fulani nalo limeonekana kuwa ni kero kubwa kutokana na ratiba za kurekodi kutokuwa katika mpangilio uliokamilika.
Hivi karibuni, muimbaji huyu wa muziki wa Injili nchini Rosemary Nyato ambaye kwa uchungu mkubwa alielezea jinsi waimbaji wanavyotabika kipindi cha kurekodi nyimbo zao, alisema kuwa, hali hiyo imekuwa kero kubwa kwa wasanii kutokana na kuwavurugia mtiririko mzima wa kuifanya kwa ufasaha kazi hiyo.
Mwanamama huyo alisema kuwa, asilimia kubwa baadhi ya studio zimekuwa zikididimiza maono ya waimbaji hasa wa muziki wa injili kutokana na kauli za nenda rudi na wakati mwingine muimbaji hujikuta anaimba akiwa amekwazika na kupelekea albamu yake itoke ikiwa katika kiwango cha chini tofauti na matarajio yake.
“Unajua mbali na tatizo la wasambazaji kutuibia kazi zetu, lakini kero nyingine ambayo imeonekana kutukatisha tamaa wasanii hapa nchini, kwa sababu wakati mwingine muimbaji huchukua mwaka mmoja akiwa studio anahangaikia suala la kurekodi pasipo mafanikio,” alisema Rose.
Muimbaji huyo aliwataka wahusika katika studio kurekebisha tabia hiyo chafu ambayo kwa namna moja ama nyingine imeonekana kuondoa utayari wa msanii kutoa kitu kilicho bora na badala yake anakuwa na bora albamu na kujikuta anapata wakati mgumu katika kuiingiza sokoni.
Rose alisema kuwa, pamoja na kwamba majira haya kuna studio nyingi ambazo zimekuwa katika hali ya kushindana kutokana na kujitangaza kupitia vyombo vya habari, lakini imekuwa ni vigumu kubaini ni studio ipi ambayo inausumbufu pindi msanii anapoenda kurekodi kazi yake.
Akizungumzia suala la waimbaji wenye majina makubwa kuwabeza wale wachanga, Rose alisema kuwa, kitendo kimekuwa kero kubwa katika huduma ya kulieneza jina la Bwana, kwa sababu Neno la Mungu limeagiza wote kuwa wamoja, lakini mambo yamekuwa yakionekana yako kinyume na maagizo hayo.
Rose alisema kuwa, waimbaji ambao Mungu amefanikiwa kuwainua kwa asilimia kubwa wamejikuta wakijikweza, hali inayopelekea hata katika matamasha hualikana wao kwa wao na kuwaacha wasanii wachanga wakihangaika licha ya kuwa na nyimbo zenye jumbe nzuri.
Aliwataka waimbaji hao waliofanikiwa kukubalika katika jamii kuwasaidia waliochini yao ili, wote kwa pamoja waweze kulihubiri vema Neno la Mungu kupitia huduma ya uimbaji.
Kana kwamba hilo hali toshi, msanii huyo alionekana wazi kukerwa na tabia ya waimbaji hao kutamka pesa kubwa pindi wanapoalikwa kwenye shughuli hasa za kiroho.
Alisema kuwa, imekuwa ni kawaida kwa waimbaji hao kutaja kiwango kikubwa cha fedha pindi wanapohitajika sehemu, ambapo nako huwa wanaimba wimbo mmoja tu na kushindwa kukidhi kiu ya watu waliomualika kwenda katika shughuli hiyo.
Katika hatua nyingi, muimbaji huyo ambaye yupo mbioni kukamilisha albamu yake aliwataka wasanii wa muziki wa injili kutunga nyimbo zenye ujumbe mzito ambao unaweza kuponya na kuwapa faraja watu waliovunjika moyo badala ya kuwa na nyimbo za kuchangamsha peke yake.
Alisema kuwa, waimbaji wengi siku hizi wamekuwa wakiangalia soko zaidi na kutunga nyimbo za kuwasisimua watu bila kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kuwa hubiri watu kwa njia hiyo ya uimbaji.
Msanii huyo alimaliza kwa kusema kuwa, waimbaji kuacha kukurupuka kwenda studio kurekodi nyimbo za ujumbe wa Mungu kwa lengo la kufanya biashara, kwa sababu hata kama muimbaji akiwa na nyimbo za taratifu watu wanaweza kuzipenda bila kuangalia ni kwa jinsi gani wanasisimka pindi wanapokuwa wanazisikiliza.
Rose alitoa mfano kwa waimbaji kama Christina Shusho, marehemu Fanuel Sedekia, Abiudi Misho na Jackson Benty ambao nyimbo zao ni za taratibu lakini zinakubalika sokoni.
Post a Comment