ROSEMARY: NITAMTUMIKIA MUNGU MPAKA SIKU YA MWISHO
WAIMBAJI wengi wa muziki wa Injili wamekuwa wakijiingiza katika huduma hiyo kwa kusaka masilahi zaidi kuliko kulihubiri neno la Mungu kwa njia hiyo.
Kutokana na hali hiyo ndiyo maana baadhi yao wamekuwa wakitunga nyimbo kwa kulenga biashara na kufanya usanii wa hali ya juu wakati wa kurekodi vibao vyao na ukivisikiliza kwa haraka utajua kama ni uimbaji ndiyo huo.
Nasema hivyo nikiwa na ushahidi wa kutosha juu ya waimbaji wa muziki wa injili ambao wameamua kuivamia huduma hiyo baada ya kuona kuwa inakubalika katika jamii ukilinganisha na muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva).
Na ukitaka kujua nyimbo za waimbaji wa muziki huo wa kumtukuza Mungu kama wanafanya kama biashara, utasikia nyimbo zinazoenda na nyakati ama matukio yanayoizunguka jamii na pindi hali hiyo ikiisha nyimbo hizo hupotea kutokana na majira yake kupotea.
Pamoja na kuwa na kundi kubwa la waimbaji ambao kila kukicha wamekuwa wakiwaza kutunga nyimbo ambazo zitawatoa kimaisha, baadhi yao wamekuwa wakimwomba Mungu awape vibao ambavyo vitafanyika msaada mkubwa kwa watu wenye matatizo mbalimbali wakiwemo waliokata tamaa ya kuishi kutokana na kuzongwa na majaribu ya kila iitwapo leo.
Miongoni mwa waimbaji ambao wanafanya huduma ya kumuimbia Mungu kwa kutumia gharama zao ili kuhubiri neno la Mungu kwa njia hiyo ni, Rosemary Nyato mpakwa mafuta wa Bwana ambaye amekubali kujitoa kuieneza injili kupitia uimbaji.
Muimbaji huyu anaweza kuwa mgeni masikioni mwa wengi, lakini ni miongoni mwa waimbaji wachache ambao wamekuwa wakisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu juu ya nini anatakiwa afanye katika kumtumikia Mola wake kwa njia hiyo.
Mpakwa mafuta huyo wa Mungu tayari amefanikiwa kurekodi albamu yake yenye vibao vinane aliyoipa jina la ‘Mbinguni si lelemama’ ikiwa katika mfumo wa audio na video ambayo ina nyimbo zilizojaa utukufu wa Mungu na hazichoshi kuzisikiliza na pia kuziangalia.
Albamu hiyo anatarajia kuizindua Oktoba 24 katika ukumbi wa chini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Azania Front jijini Dar es Salaam, na shughuli hiyo itasindikizwa na wakali wa muziki wa injili nchini kama Christina Shusho, David Robert, Trenet Band, The Voice na Upendo Safari.
Alizitaja nyimbo zilizomo ndani ya albamu hiyo kuwa ni Toa sadaka, Dunia imeharibika, Ibilisi mjanja, Mbinguni si lelemama, Bariki, Kizazi cha ukaidi, Maisha ya mwanadamu na Ndoa.
Rose alimaliza kwa kusema kuwa atamtumikia Mungu wake mpaka mwisho wa maisha yake kwa maana anatambua kuwa amepewa kipawa cha kutunga na kuimba nyimbo za injili ili zifanyike msaada kwa watu wengi wanaoshi maisha yasiyompendeza Mola pamoja na wanaoishi maisha ya shida.
Wasiliana naye kwa +255 713 864539/ +255 755 333332
Post a Comment