Maharamia wa Kisomali wakamata meli mbili zaidi.
Maharamia wa Kisomali wameteka nyara meli mbili zaidi za mizigo katika ghuba ya Aden katika bahari ya Hindi siku ya Jumatatu. Kukamatwa huko kwa meli ya Uingereza ya St. James Park , na meli ya mizigo ya Panama , Navios Apollon , kuna maana wahalifu hao wa Kisomali hivi sasa wanashikilia kiasi ya meli 11 na karibu mabaharia 250. Miongoni mwa wale wanaoshikiliwa ni pamoja na raia wawili wa Uingereza mke na mume waliokamatwa mwezi wa Oktoba wakati wakisafiri na meli yao kwenda Tanzania. Maharamia wamepata mamilioni ya dola kutokana na kuteka nyara meli na kulipwa fedha nyingi katika ghuba ya Aden, ambayo inaunganisha bara la Ulaya na Asia. Majeshi ya majini ya nchi za kigeni pamoja na yale ya umoja wa Ulaya yameweka meli zao za kivita katika eneo hilo ili kulinda meli za kibiashara lakini eneo hilo kubwa ambalo linahitaji kufanyiwa doria linaendelea kuwa hatari kwa meli nyingi.
Post a Comment