Waratibu wa misaada wilayani Kilosa wafundwa
SERIKALI imewatahadharisha wanaoratibu misaada ya waathirika Kilosa kuepuka kutumia ovyo misaada hiyo ili wasikumbwe na kashfa baadaye.
Tahadhari hiyo ilitolewa juzi na Makamu wa Rais Dk Ali Mohammed Shein wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kiwanja cha Shule ya Msingi ya Kilosa Town .
Makamu wa Rais alifanya ziara ya siku moja juzi wilayani humo ambako alikagua maeneo mbalimbali yaliyokumbwa na mafuriko hayo pamoja ma kambi za muda za kuhudumia waathirika hao za Kibamba, Mazulia na Shule ya Msingi Kilosa Town .
"Wito wangu kwenu mliokabidhiwa kuratibu na kugawa misaada kwa wenzetu walioathirika mfanye kazi yenu kwa uadilifu na kwa kuwaonyesha upendo wenzetu hawa na bila ya kufaulisha misaada hiyo"alionya Dk Shein na kuongeza kuwa waliokabidhiwa jukumu hilo wamepewa heshma kubwa hivyo waithamini.
Dk Shein aliwahakikishia wananchi wa Kilosa kuwa serikali hatua kwa hatua itarejesha huduma wilayani humo ikiwemo ya kurejesha miundombinu ikiwemo sehemu ya reli iliyoharibika ili maisha yao yaweze kurejea katika hali ya kawaida.
"Tutawaletea huduma hatua kwa hatua hadi pale maisha yenu yatakapotengemaa na tunafanya hivyo kutimiza wajibu wetu wa kuwahudumia kama tulivyoahidi katika kampeni zetu za uchaguzi,"alibainisha
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa Kilosa, Makamu wa Rais aliwapongeza askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) kwa kazi nzuri lililoifanya katika kusaidia urejeshaji na upatikanaji wa huduma kwa wathirika wa mafuriko hayo huku akiwataka wananchi nao kutobweteka badala yake waunge mkono askari hao kwa kufanya kazi wanazoziweza.
"Kwa upande wetu sisi waathirika tuangalie kile tunachoweza kukifanya kuwasaidia wanajeshi wetu,nanyi tekelezeni wajibu wenu,mkiwa bega kwa bega nao watapata moyo na kufanya kazi kwa bidii zaidi"aliwaeleza wananchi na kuwataka waendelee kushirikiana bila ya kujali itikadi au jinsia wakati huu kama ilivyo wakati mwingine.
Dk Shein aliwataka wananchi hao kuendelea na shughuli zao za kawaida kila wanapopata nafasi katika kipindi hiki wakiwa katika makazi ya muda na kuutaka uongozi wa Wilaya na Halmashauri kuhakikisha inawapatia wananchi hao mbegu bora za mazao.
Kufuatia athari zilizosababishwa na mafuriko hayo, Dk Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa ni nafasi ya kujikumbusha umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya wataalamu katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya na ujenzi.
Wakati huo huo Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alitoa wito kwa wananchi wa Kilosa hasa walioathirika na mafuriko kuwa pamoja na kuwepo kwa misaada mingi, lakini wasisahau kuendelea na shughuli zao za kujipatia kipato hata kama bado wataendelea kuwa katika makambi ya muda.
Habari hii ni kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi
Post a Comment