Frank John Litambo ‘Mungu akikuinua hakuna wa kukushusha’
Muziki wa Injili unaendelea kujipatia mashabiki wengi hapa Tanzania kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika kwa mfano, Afrika Kusini , Nigeria , Kenya , Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambazo miaka ya hivi karibuni zimekuwa ni mifano bora kwenye maendeleo ya muziki huo.
Kwa sasa waimbaji wengi wa Kitanzania wameendelea kufuata za nyayo za wakali wengine wakubwa dunia kama Marymary, Makoma, Midnight Crew ambao kwa kiwango kikubwa wamekuwa ni mifano kwa waimbaji wa maeneo mengine duniani.
Mwinjilisti Frank John Litambo ambaye ni mmoja wa waimbaji wa muziki wa Injili hapa Tanzania kwa kuda mrefu sasa ameendelea kufanya harakati kwenye muziki huo kwa kushirikiana na waimbaji wengine wa ndani na nje ya taifa hili.
Akizungumzia harakati zake ndefu na mafanikio ambayo ameyafikia, Litambo anasema kuwa kuna mengi amepitia lakini anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kuendelea kuifanya kazi hiyo kwa mafanikio licha ya vikwazo mbalimbali alivyokutana navyo.
“Nina kila sababu ya kushukuru kwa maana hatua hii niliyofikia si jambo rahisi naamini kuwa Mungu akiamua kukupandisha hakuna anayeweza kukushusha.
“Kwa mantiki hiyo ni wazi kuwa kuingia kwangu kwenye muziki wa Injili halikuwa ni jambo la kutaka ila ulikuwa ni wito kutoka kwa Mungu, ndiyo sababu nimeendelea kuwepo hadi sasa,” ameongeza muimbaji huyo ambaye yupo ndani ya fani hiyo kwa miaka sita sasa.
Baada ya kufanya utumishi huo kwa muda mrefu hivi sasa Muinjilisti Litambo ametoka tena na kazi mpya ikiwa ni ya pili ambayo tofauti na kazi nyingine ameamua kufanya uzinduzi kwa njia ya hisani kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa masikio (viziwi) utakaofanyika Mei 9 mwaka huu.
“Katika albam yangu hii uzinduzi wake utakuwa ni tofauti kwa kuwa nimelenga kupeleka fedha kwa watu wenye matatizo katika jamii, miongoni mwao ni watoto wasiokuwa na uwezo wa kusikia.
“Kwenye jambo hili nimeshirikiana na viongozi wa dini na wanasiasa ili kulifanikisha naamini huu ni mchango wao mkubwa katika jamii inayowazunguka,” amefafanua muimbaji huyo.
Ndani ya hafla hiyo atasindikizwa na waimbaji mbalimbali wa Injili kutoka Tanzania ambao ni Ambwene Mwasongwe, Sifa John, Victor Aron, Catherine Ntepa, KKKT Unjilisti Kijitonyama na The Messengers Band.
Katika albam hiyo ya pili kwa Muinjuilisti huyo imebeba jumla ya nyimbo nane ndani yake ambazo baadhi yake ni Mama, Atatufuta Machozi, Yatima, Ndoa na nyingine nyingi.
Post a Comment