MARTHA ESAU MWAIPAJA: NACHUKIZWA NA DHAMBI YA NGONO
Kuokoka si kazi ngumu bali kuutunza wokovu ndiyo kazi. Leo hii si jambo la ajabu kusikia mtu amesimama madhabahuni na kutangaza kuwa ameokoka na kupigiwa makofi na waamini kutokana na uamuzi huo. Lakini siri ya wokovu hubaki moyoni mwa mhusika.
Kama nilivyotangulia kusema mwanzo kuwa kuokoka si kazi ngumu bali kuutunza wokovu. Sio jambo la kushangaza kusikia Mchungaji, Padiri, Askofu, Mwinjilisti kusikia ana nyumba ndogo.
Lakini si watumishi hao tu, bali hata waimbaji wa muziki wa Injili nao wanaandamwa na tatizo la uzinzi. Baadhi ya waimbaji ukisikia nyimbo zao utafikiri kuwa wao wako rohoni kweli lakini ukweli ni kwamba kitu ambacho hufanyika hapo ni usanii mtupu.
Kwani baadhi ya waimbaji wa muziki huo wenye kumtukuza Mungu wamekumbwa na tatizo la kupenda ngono pamoja na mambo mengine kama mtu asiyeokoka. Kuna mifano mingi ya waimbaji wa muziki wa Injili ambao wanafanya mambo yaliyokinyume na mwenendo wa Mungu.
Lakini pia wapo waliosimama katika kweli ya Mungu. Miongoni mwa hao ni Martha Esau Mwaipaja ambaye anakuja kwa kasi ya ajabu kunako muziki wa Injili. Martha mwenye sura ya upole aliniambia juzikati kuwa, anachukizwa sana na wasanii wenzake wanaofanya dhambi hasa ya uasherati na uzinzi kwani kufanya hivyo ni chukizo mbele za Mungu.
“Nachukizwa na dhambi ya ngono kwani kufanya hivyo kunaweza kuniweka mbali na Mungu wangu. Lakini si ngono pekee bali kila dhambi kwani siwezi kwenda mbinguni kwa sababu ya kuimba nyimbo za Injili,” alisema dada huyo ambaye kibao chake cha ‘Tusikate Tamaa’ kimewakamata watu wengi.
Martha mwenye miaka 22 alidai kuwa maisha yake yote anamtegemea wokovu kwani ndiyo dira yake ya kumwezesha kufanikiwa kwa kila jambo, kwani muda mwingi atakuwa karibu na Mungu hivyo itakuwa rahisi kujibiwa mahitaji yake atakayokuwa anayomba kutoka kwa Muumba wake.
“Mungu anasema ukimheshimu naye atakuheshimu, sipendi niwe kama bango la kuwaelekeza watu kwenda kwenye uzima wa milele halafu mimi niende jehanamu. Nawaomba waimbaji wenzangu wanaofanya mambo ya kumchukiza Mungu wasifanye hivyo ili wawe mfano mzuri katika jamii kwa kuishi maisha matakatifu,” alisema Martha.+
Akieleza sababu za waimbaji wa muziki wa Injili kuelemewa na dhambi ya uzinzi, uasherati pamoja na nyingine alisema kuwa, wengi wao hawapati muda wa kuwa karibu na Mungu ndiyo maana Shetani anatumia mwanya huo kuwarubuni na kujikuta wanafanya hivyo bila wao kujijua kwani wakati huo ufahamu wao huwa umefungwa.
Alimaliza kwa kuwataka waimbaji wenzake kuwa na umoja ili kudhihirisha ukweli kwamba wao ni watumishi wa Mungu wanaositahili kuigwa jamii inayowazunguka.
Post a Comment