Stara Thomas atoswa tamasha la Pasaka
KAMATI ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka, imemtosa mwanamuziki nguli wa zamani wa muziki wa Bongo Fleva, Stara Thomas, aliyetangaza kuokoka hivi karibuni na kuomba atumbuize kwenye tamasha hilo la nyimbo za injili ambalo hufanyika kila mwaka.
Habari kutoka ndani ya Kamati hiyo zinaeleza kuwa kutoswa kwa msanii huo kunatokana kushindwa kubaini vema mienendo ya mwanamuziki huyo ambaye amedai ameanza kutunga nyimbo za Injili. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Alex Msama, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa hayo ni maamuzi ya Kamati yake. Tamasha la Pasaka la kumsifu Mungu linatarajiwa kufanyika Aprili 24, mwaka huu kwenye ukumbi wa Dimond Jubilee, Dar es Salaam. Hivi karibuni Stara alikaririwa na vyombo vya habari kuwa anaamini Mwenyezi Mungu atamwongoza kutengeneza albamu ya Injili itakayokuwa ya shukrani kwa Muumba wake. Mwanamama huyo awali alikuwa akiabudu katika Kanisa la Jamatrine, lakini kwa sasa tangu 'azaliwe upya', anaabudu katika Kanisa la Shalom lililoko Mbezi Salasala. Msanii huyo alisema kujikita kwake kwenye muziki wa kiroho, kuna maana kwamba, ameachana na muziki wa kidunia, na hatatunga tena nyimbo za aina hiyo. Stars alitamba na nyimbo za Bongo Fleva kama Sikia, Sitorudi Nyuma, My Body na Children's Right, alizozipiga katika miondoko ya Zouk. Hivi karibuni alivuma na wimbo wa Nipigie alioshirikiana na AT. Stara alianza kuchomoza zaidi kimuziki mwaka 2000, alipoibuka na nyimbo za Sikia, Mimi na Wewe, zilizokuwa katika albamu ya Nyuma Sito Rudi. Kipaji chake kilidhihirisha mafanikio ambapo mwaka 2003, Stara alishinda tuzo ya Kilimanjaro Music Award kwa kuwa Mwimbaji Bora wa Kike Tanzania. Stara ambaye ni mwenyeji wa Mwanza, mwaka 2004, alitoa albamu ya Hadithi, ikiwa ni albamu yake ya pili. Alianza kuimba akiwa na umri wa miaka saba, tangu akiwa shuleni. Picha kwa hisani ya Strictly Gospel.
Post a Comment