JANETH JONAS MREMA MWIMBAJI WA NYIMBO ZA INJILI (THE HEALING VOICE)
YAJUE MAISHA YAKE, WAPI AMETOKEA NA ANAKOENDA
Janeth ni mtoto wa kwanza wa familia ya Mzee Elly Temu na marehemu mama Veronica Bagenyi. Baba yake alizaliwa Marangu Moshi kijiji cha Komalyangoe na mama yake alizaliwa mkoani Kagera Wilaya ya Karagwe kijiji maarufu cha Kaisho. Aidha katika tumbo la mama yake wamezaliwa watoto wanne wa kike wawili (2) na wa kiume wawili (2) wengine ni Lucas, Eric na Catherine.
ELIMU
Janeth Mrema alihitimu elimu ya msingi katika shule ya msingi kiwanja cha Ndege Area C Dodoma mwaka 1991, alifaulu na kuchaguliwa kujiunga shule ya Sekondari ya Dodoma na kuhitimu kidato cha nne (O-Level) mwaka 1995, hapo pia alifaulu na kuchaguliwa kujiunga na shule ya wasichana Ashira iliyopo eneo la Marangu mkoani Kilimanjaro ambapo alihitimu kidato cha sita mwaka 1998. Mwaka 1999 dada Janeth alijiunga na na chuo cha Biashara kampas ya Dodoma kwa ajili ya elimu ya juu ambapo mwaka 2002 alihitimu na kutunikiwa Stashahada ya juu ya uongozi wa biashara ( Business Administration), aidha Janeth amekuwa akivutiwa na mambo ya ujasiriamali na uongozi hivyo ameendelea kuhudhuria kozi mbalimbali zinazohusu mambo hayo ili kujinoa zaidi, pamoja na huduma ya uimbaji, Janeth na mumewe Jonas wanajishughulisha na shughuli za ujasiriamali.
JANETH NA UIMBAJI
Kipaji chake cha uimbaji, walianza kukigundua walimu wake wa shule ya Jumapili (Sunday School) katika kanisa la KKKT usharika wa Arusha road Dodoma, na kati yao hakusita kuwataja mwalimu Alexander Lyaro na Mchungaji Menard Kipyali ambaye pia alihusika sana kukinoa kipaji chake baadaye alipojiunga na kwaya ya vijana.
Akiwa darasa la saba Janeth alichaguliwa na walimu wake wa shuleni kutunga wimbo ambao uliimbwa katika maadhimisho ya UMISHUMTA 1991, ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Dodoma kwa mwaka huo.
Akiwa Sekondari alishika vyeo mbalimbali kama katibu wa Ukwata Dodoma Sekondari, Mwenyekiti msaidizi wa Ukwata akiwa Ashira High School, na katibu wa Tafes alipokuwa chuoni. Mwaka 2001 aliweza kuwa mwakilishi katika mkutano mkubwa wa vijana EZRA Conference uliofanyika Nairobi nchini Kenya, na katika mambo yote hayo msukumo mkubwa ulitokana na huduma yake ya uimbaji.
Baada ya kuolewa Janeth na familia yake ni washiriki wa kanisa la Kibaptisti Magomeni jijini Dar es Salaam, chini ya Mchungaji Anyingisye Mwasandube, ingawa huduma ya uimbaji inawapa nafasi ya kushiriki makanisa na huduma mbalimbali.
MSAMBAZAJI NA UPATIKANAJI
Watu mbalimbali walimtia moyo na kumhimiza Janeth kuingia studio, na hilo limewezekana, Janeth amefanya albam nzuri sana mwanzo mpaka mwisho yenye nyimbo maarufu kama Piga Makofi, Mbona washika tama, Sala yangu, Nakuhitaji Roho n.k ambayo sasa imeingia sokoni na inasambazwa na UMOJA AUDIO VISUAL na GMC wasanii promoters na inapatikana katika Audio tape, Audio Cd, Vcd na Dvd.
UZINDUZI
Albamu ya piga ya PIGA MAKOFI itazinduliwa rasmi siku ya Jumapili ya tarehe 29 May 2011 katika ukumbi mwanana wa Ubungo Plaza kuanzia saa 7:45 Mchana.
Uzinduzi huu utakuwa ni wa aina yake kabisa na utahudhuriwa na wageni mbalimbali mashuhuri wakiwemo, wanasiasa, wafanyabiashara, watumishi wa Mungu na wakurugenzi wa makampuni mbalimbali. Aidha dada Janeth anapenda kuwakaribisha watu wote wa dini na madhehebu yote kuhudhuria tamasha hilo kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
Waimbaji mbalimbali wa ukweli watakaotinga ndani ya ubungo Plaza kumtia joto mwenzao ni pamoja na ile bendi maarufu inayoimba nyimbo za Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa n.k, ijulikanayo kama the Messengers Band, bila kuwasahau The TM Music waimbaji wa kimataifa wenye vipaji vya ajabu ambao wanaimba kwa style ya Congregational Singing (uimbaji wa watu wengi) kikundi hiki kina waimbaji wengi zaidi ya watu 200, pia kwaya mbalimbali zitakuwepo.
Waimbaji binafsi ni pamoja na Martha Mwaipaja, Stella Joel, Ningile Mwakatage, Kanuni Kayombo, Addo November, Upendo Nkone, bila kumsahau mwana mama Christina Shusho.
KIINGILIO
Kiingilio katika uzinduzi huo kimeshushwa ili kila mtu aweze kuhudhuria hivyo kitakuwa shilingi elfu tano kawaida na elfu kumi viti maalumu usingoje kusimuliwa, njoo ushuhudie mwenyewe, na Mungu akubariki, Amina.
Post a Comment