The Holly Family Gospel Singers: Injili itolewe bure kwa ajili ya wote
KUNDI la muziki wa Injili la Makoma la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limeendelea kuwa kundi bora la muziki wa Injili katika maeneo mbalimbali Afrika na duniani kote.
Kwa Tanzania yapo makundi mengi yanayofanya muziki wa aina hiyo likiwemo, J-Sisters, Rafiki Gospel Singers na mengine mengi ambayo kimsingi yanachangia kuongeza ukuaji wa muziki huo hapa nchini.
Lakini kwa hivi sasa mambo yanaonekana kuwa mazuri zaidi katika muziki huo baada ya Kundi la The Holly Family Gospel Singers kuonekana kuchomoza kwa kasi kwenye ulimwengu wa muziki huo huku likikubalika ndani na nje ya Tanzania kiwepesi.
Wakielezea mwenendo wao katika muziki wa Injili, waimbaji hao wanasema kuwa pamoja na kuwepo kwenye fani hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu sasa lakini bado wameendelea kukumbana na changamoto zilizopo kwenye fani hiyo kutokana na ukweli kwamba ni kazi ambayo inapigwa vita na shetani.
“Kazi hii si lelemama kuna majaribu mengi yanatukumba, ila tunamshukuru Mungu kwa kuwa ameendelea kutusimamia na kutupigania siku hadi siku kwani kama ingekuwa ni kwa nguvu zetu tusingeweza kufika popote,” anasema Ester Ntobi ambaye ni binti pekee kwenye kundi hilo lenye waimbaji watano.
Ntobi kwa niaba ya wenzake amefafanua kuwa, pamoja na changamoto zinazowakabili lakini wanamshukuru Mungu kuwapa kibali mbele za wanadamu kwani wamekubalika ndani na nje ya Tanzania, hii ni baada ya kupata mialiko mingi kwenye matamasha ya muziki huo.
Miongoni mwa mambo ambayo wanaona ni faraja kwao ni kupewa nafasi ya kufika katika maeneo mengi ambayo waimbaji wengi wamekuwa hawafiki au Injili imekuwa hasifiki mara kwa mara kutokana na mazingira au tamaduni za wanajamii husika.
“Kwa mfano, Zanzibar, Mafia na Mtwara ni maeneo ambayo tumekuwa tukienda mara kwa mara kwa ajili ya kufanya huduma ya kulitangaza Neno la Mungu, maeneo haya yamekuwa hayafikiwi na waimbaji wengi,” anafafanua Emmanuel Kapandila ambaye ni kiongozi wa kundi hilo.
Kadhalika siku chache zijazo wanatarajia kufanya ziara katika nchi za Uganda, Rwanda na Burundi, hii ni baada ya kupata maombi kutoka kwa makanisa ya Kikatoliki ya miji ya Jinja, Kampala, Kigali na Bujumbura na baadaye kwenda jijini Stockholm nchini Sweden na kisha mwakani wataelekea nchini Israel kwa ajili ya shughuli za hija katika miji mitakatifu ikiwemo mji wa Yerusalem.
Mbali ya mafanikio hayo, waimbaji wa kundi hili wanaeleza kwamba kuna mambo kadhaa ambayo wanaamini yanawakwamisha kwenye mikakati yao ya , hivyo serikali inatakiwa kuyaangalia kwa makini ili wanaovuja jasho waweze kunufaika na kile wanachokifanya.
“Ndugu yangu kwenye muziki wa Injili kuna matatizo mengi lakini tunachokiona hapa ambacho ni kilio cha watu wengi ni jinsi ambavyo kazi zetu zinavyoshindwa kutunufaisha, nadhani mimi nikiwa ni muinjilisti sitaki kutumia huduma hii kama biashara, lakini tunachohitaji ni kuhakikisha kazi yetu inawafikia watu wengi tena ikiwezekana bila malipo kwani hiyo ndiyo maana halisi ya Injili ya Yesu Kristo,” anaeleza Kelvin Hayola, ‘Black’.
Kundi hilo kwa sasa lina albamu moja iitwayo Nitakusifu yenye nyimbo nane, baadhi ya nyimbo hizo ni Nitakusifu, Bwana Unifadhili na Maombi Yangu zimeweza kulitangaza vema kundi hilo katika medani ya muziki wa Injili, ambalo kwa sasa lipo kambini likiandaa video ya albamu hiyo.
Post a Comment