MARTHA MHANZE: Uimbaji wa Injili unahitaji utakatifu
Kwa leo nimebahatika kukutana na Mtumishi wa Mungu, Martha Nelson Mhanze, mwenyeji wa Moshi japo kwa sasa makazi yake yapo jijini Dar es Salaam ambapo ameamua kumtumikia Muumba wake kwa njia hiyo kwa lengo la kuwafikia watu wengi.
Martha anasema kuwa, muda mwingi amekuwa akitamani kuhubiri Neno la Mungu kama mhubiri lakini anashindwa kufanya hivyo kutokana na sababu ambazo binafsi hazifahamu, na ili kiu yake ya kueneza injili isizimike, ameamua kutumika kwa njia ya uimbaji.
Na kwa kudhihirisha kwamba kweli Mungu amemuita kumtumikia, Martha tayari amekamilisha albamu yake yenye nyimbo tisa inayokwenda kwa jina la Mnawaza Nini ambayo imefanyika baraka kubwa katika jamii kutokana na ujumbe mzito uliomo ndani ya vibao hivyo.
Martha amabye ni mke wa mme mmoja na watoto watatu, aliiambia safu hii kuwa, Jehova amekuwa akimtumia ipasavyo kupitia wimbo wake wa Mnawaza Nini, ambapo siku moja aliuimba katika madhabahu moja jijini Dar es Salaam na mama mmoja aliyekuwa anasumbuliwa magonjwa mbalimbali alijikuta anapona na kumrudishia Mungu utukufu kutokana na kitendo hicho.
Baada ya kunipa ushuhuda huo wa mgonjwa kuponywa magonjwa yake kupitia wimbo huo, nilitaka kujua ni kwanini mgonjwa huyo apone kupitia wimbo huo badala ya kuombewa na wachungaji kama ilivyozoeleka. Martha alisema kuwa, binafsi amekuwa akiimba kwa kumaanisha, na muda mwingi amekuwa akimwomba sana Mungu wake ili watu wahudumiwe kupitia nyimbo zake.
“Uimbaji wa muziki wa injili unahitaji utakatifu, na muda wote unatakiwa uwe karibu na Mungu ukimuomba akusaidie kulihubiri Neno lake kwa njia hiyo ya uimbaji na watu wapate uponaji kwa kusikiliza nyimbo badala ya kusubiri mpaka waende kuombewa na wachungaji, askofu, wainjilisti na mapadri, kumbe hata kwa kusikiliza nyimbo tu wanaweza kuhudumiwa.
“Jambo hilo haliwezi kufanyika kama mhusika asipokuwa mtakatifu, kwa sababu baadhi ya waimbaji wa muziki wa injili wamekuwa wakijisahau kutulia uweponi kwa Mungu badala yake wamekuwa wakijichanganya na mambo ya dunia na kuifanya huduma hiyo ionekane si kitu huku baadhi ya nyimbo zikionekana kupigwa kwenye kumbi za starehe kama burudani pekee,” alisema Martha.
Albamu ya mtumishi huyo wa Mungu yenye nyimbo kama Dunia yapita, Yesu wangu nakupenda, Mnawaza nini?, Baba tunaomba rehema, Kumbuka, Maisha, Nijapopita, Basi wamwitaje? na Baba yetu, tayari iko sokoni ikiwa katika mfumo wa kaseti (audio), CD, VHS, VCD na DVD na imezinduliwa hivi karibuni.
Na ili kudhihirisha kwamba yeye ameitwa na Mungu wake, zoezi la kuiandaa albamu hiyo limechukua muda mrefu. Kwa mara ya kwanza aliingia studio mwaka 2007 akarekodi audio CD, na mwaka 2008 alianza kazi ya kurekodi video na ilichukua mwaka mzima, na baada ya hapo aliendelea kuiweka mikononi mwa Mola na mwishoni mwa mwezi uliopita akaamua kuizindua.
Martha alimaliza kwa kuwataka waimbaji waliofanikiwa kupata majina katika anga za muziki huo kuacha kudai kiasi kikubwa cha fedha pindi wanapoalikwa kwenye shughuli ya kumtukuza Mungu, na wakumbuke kuwa Mola ndiye aliyewapa huduma hiyo na ana uwezo wa kuwapokonya na kubaki watupu.
Post a Comment