Nabii Viacent: Maslahi ya Mungu ni bora kuliko ya Wanadamu
Leo nimefanikiwa kuzungumza na muimbaji wa kimataifa wa muziki wa Injili kutoka nchini Kenya , ambaye pia ni Nabii, Viacent Mtokambali, ambaye nimezungumza naye kuhusu masuala mengi ya msingi yanayohusu huduma yake ya kumuimbia Mungu na kulihubiri Neno lake.
Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara nyingi kupitia safu hii, imebainika kuwa, baadhi waimbaji wameivamia huduma hii kwa kuangalia maslahi yao binafsi na wala si kulihubiri neno la Mungu kama wanavyopaswa kufanya.
Leo hii si ajabu kuona muimbaji akikataa kutoa huduma ya uimbaji kwenye mikutano na mikusanyiko ya kidini, mpaka alipwe kiwango cha fedha anachokitaka, na hata kama atapewa, akifika sehemu husika huimba wimbo mmoja na kisha kuondoka hata kabla ya mkutano kumalizika.
Sasa, iweje udai fedha kubwa kwa ajili ya kwenda kutoa huduma ya uimbaji kwenye mkutano, huku ukipewa nafasi ya kuimba unaimba wimbo mmoja kisha unaondoka zako? Kwanini usikae mpaka mwisho wa mkutano na wewe ukashiriki kutoa huduma kwa watu wenye matatizo mbalimbali kutokana na nafasi yako ya utumishi?
Swali hili nilimtupia muimbaji Mtokambali ambaye ni raia wa Tanzania , mzaliwa wa Mwanza ambaye anafanyia kazi zake nchini Kenya , naye bila hiyana alinijibu kuwa, yeye binafsi huwa anathamini huduma kwanza na masuala mengine yanafuata baada ya shughuli, kwa sababu imempasa mtumishi kula vya madhabahuni kwake.
“Swali hilo kaka ni zuri, biblia inasema kwamba, wataendaje wasipopelekwa, hii ina maana kuwa huwezi kuwa na ujasiri wa kusafiri kwenda sehemu kutoa huduma, kama hujawezeshwa, wakati mwingine unalazimika kwenda mikoa ya mbali. Kwa kuwa hiyo ni moja ya huduma, ni vyema wahusika wakapewa ujira waojapo kidogo ili kuwawezesha kutenda kazi ipasavyo.
Pamoja na hayo, mimi binafsi maslahi ya Mungu ni bora kuliko ya wanadamu. Hata biblia inasema kuwa; Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote akipata hasara ya nafsi yake? Marko 8:36. Natambua Mungu ana njia nyingi za kumfanikishia mtumishi wake atakapomuona anaifanya kazi yake kwa uaminifu,”.
Mtokambali alisema kuwa, anachohitaji yeye ni kuona anapata habari za watu kupokea uponyaji kupitia ujumbe unaopatikana kupitia nyimbo zake. Akazidi kuleza kwamba, nyimbo zake zimepelekea kufanyika kwa baraka kubwa katika jamii, na kwa kiasi kikubwa amepiga hatua kiroho kwani amekuwa akizungumza na Mungu wake mara kwa mara kila anapoona kuna jambo linamsumbua na Mungu humsaidia kupata majibu yake.
Nabii Mtokambali, yupo nchini akijiandaa na uzinduzi wa albamu yake ya kwanza aliyoipa jina la ‘Nilipotea’ yenye nyimbo nane na shughuli hiyo inatarajiwa kufanyika Desemba 20 mwaka huu, katika Ukumbi wa Friends Corner jijini Dar es Salaam .
Nyimbo zilizomo ndani ya albamu hiyo ni pamoja na Wapendwa, Wanadamu, Nimempata, Nilipotea, Mkono wa Baba, Vita kali, Yalitabiriwa na Ole wako.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo ni Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azzan akisindikizwa na Waziri wa Maendeleo, Mifugo na Uvuvi, John Pombe Magufuli, Anton Lwegamba na Laurence Chitalilo.
Nabii huyo alianza rasmi shughuli ya kumuimbia Mungu mwaka 2004, akiwa kijijini kwao Mwagika, mkoani Mwanza, kabla ya kutimkia nchini Kenya akiambatana na ‘wamishonari’ kutoka Denmark waliokunwa na kipaji chake baada ya kumuona anaimba kwa ufasaha kwenye kwaya moja jijini Mwanza.
Post a Comment