KATIBA MPYA – INAWEZA KUTAFSIRIWA KUWA FIMBO YA MNYONGE
Usiku na mchana majumba yanaporomoka Nairobi , Kiambu, Mombasa na kwingineko nchini huku ikisababisha maafa na hasara tilatila. Lakini bado serikali inaendelea kukubali au kuvumilia kubaki na kuendelea kujengwa kwa nyumba na majumba ambayo yanaweza kuporomoka wakati wowote ule. Je, kwa mfano, mtetemeko wa ardhi kama ule wa Haiti ukitokea Nairobi , itakuwaje tukikumbuka kuwa asilimia kubwa zaidi ya nyumba zimejengwa kinyume cha sheria, na ni makaburi hasa yanayongojea kuwazika wakaazi wa jiji wakati wowote? Mbona serikali inaangalia huku mitaa ya mabanda iliyojaa majumba mabovu na hatari ikichipuka kila siku?
Turudi kwa swala la katiba. Nimekuwa nikikariri kuwa lazima tupate katiba mpya mwaka huu. Ndiyo kwa sababu nakubaliana na wale wanaopendekeza bunge libadilishe sheria ili tupigie kura katiba mbili wakati mmoja katika kura za maoni. Swala nyeti zaidi linalotisha kutuzuia kupata katiba mwaka huu ni lile la mfumo wa utawala, uwe wa urais ama wa ubunge? Basi tupige kura za kuchagua kati ya katiba mpya yenye mfumo wa urais au yenye mfumo wa ubunge. Tusikose katiba mpya mwaka huu. Tupate fursa ya kuanza kuitumia katiba mpya kupambania mfumo mpya wa kijamii-kiuchumi utakaohakikisha kukua kwa utekelezaji wa haki za binadamu kwa maneno na vitendo.
Sura ya sita ya ruwaza ya katiba ya kamati ya wataalamu wa katiba inahusu haki za binadamu. Sehemu ya pili ya suraha hii inatoa orodha ndefu ya haki za binadamu. Jambo hili ni muhimu maana haki za binadamu ndiyo mama wa mambo yote. Aidha, shabaha ya kimsingi ya siasa, uchumi, matumizi ya ardhi na rasilimali, maendeleo, demokrasi na utawala, ni kukua kwa utekelezaji wa haki za binadamu. Hata hivyo, ingawa haki za binadamu ni za kila binadamu, katika jamii iliyogawanyika kitabaka kama ya Kenya , hapawezi kuwa na usawa katika utekelezaji wake hata katiba ikisema hivyo. Maana tajiri na maskini kamwe hawawezi kutekeleza haki kwa usawa wakati mmoja. Ndiyo kwa maana harakati za kitabaka huhusu mapambano ya haki ya kutekeleza haki za binadamu katika jamii.
Haki zako za binadamu ni yale mambo yote ambayo ni yako kwa kuwa u binadamu. Wala hailetwi na katiba. Kwani ulikuwa na haki zako za binadamu mara tu ulipozaliwa, kwa sababu tu wewe ni binadamu. Kwa mfano, maisha ni haki yako ya binadamu, tena ya kimsingi. Hii ina maana kwamba kwa sababu tu umezaliwa, upo, u hai, maisha ni haki yako. Wala huhitaji kuomba ruhusa kutoka kwa mtu yoyote yule ili uishi. Isitoshe, hakuna mtu yoyote yule alie na haki juu ya uhai wako, hakuna mwenye haki halali ya kukuzuia kuishi, ya kukua. Na endapo mtu akakuua kwa sababu yoyote ile, basi atakuwa amekunyang’anya haki yako ya kimsingi, uhai.
Ruwaza ya katiba ina orodha ya haki za binadamu, uhuru wa maisha, usawa, haki za watoto, haki za wazee, haki za vijana, haki za wafanyikazi, haki za huduma ya jamii, haki ya elimu, haki ya matibabu, haki ya chakula, haki ya nyumba, haki ya maji, haki ya mazingira bora, n.k. Orodha yenyewe ni ndefu. Kumunyima mtu haki zake za binadamu ni kumdhulumu, kumvua utu wake, ni kuvunja haki za binadamu. Lakini tunajua kuwa nchini idadi kubwa zaidi ya watu hawatekelezi haki hizi kutokana na imla, ubepari na kiwango cha maendelo na uhuru wa nchi yetu. Haki za binadamu zina historia, zimekuwa zikizidi kutekelezeka kufungamana na kukua kwa maendeleo na uhuru katika jamii.
Ikitafsiriwa kimaendeleo, kutokana na msimamo wa wengi, orodha ya haki za binadamu iliyoko katika ruwaza ya katiba, itatumiwa kuhalalisha mapambano ya kuleta mfumo mpya na wa hali ya juu zaidi utakaoleta usawa katika utekelezaji wa haki za binadamu, ujamaa. Na njia ya mkato ya kuhakikisha ahadi za haki za binadamu zilizoko kwa ruwaza ya katiba zinatekelezwa ni kwa kila anaenyanyaswa kujitayarisha kujiandikisha na kupiga kura za mageuzi mnamo mwaka wa 2012. Kila mzalendo awajibike. Tuondoe wezi, waporaji wa mali ya umma, matapeli, wabakuzi wa ardhi, wafisadi, wauwaji, wanaoharibu mazingira, vibaraka wa mabeberu na mabepari.
Tujitokeze, tupige kura kwa kuchagua sera za haki na ukombozi wa wengi wala siyo ukabila, hongo, malalamiko matupu au kutojali. Tukumbuke wale tutakaowachagua kuwa viongozi wa taasisi zote za dola na serikali zitakazokuwapo katika katiba mpya, ndiyo watakaokuwa na fursa kuongoza jamii kutafsiri na kutekeleza orodha ya haki za binadamu katika maisha halisi nchini. Tusisahau, mbele ya mwenye nguvu, mnyonge hana haki. Tutahadhari na waliyoko madarakani leo. Fimbo ya mnyonge ni muungano wa wanyonge wa kupigania ukombozi wao wenyewe. Tunaweza kutumia katiba mpya kama fimbo ya mnyonge ya kuwaunganisha wenye lengo la kupambania na kuleta dola la kutumia rasilimali za kitaifa kufanya shabaha ya maendeleo kuwa ni kuongeza utekelezaji wa haki za binadamu za kila Mkenya.
Makala ya Nguvu ya Hoja imeandikwa na Mwandawiro Mghanga , wa KSB Nairobi, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com.
Post a Comment