Mtikila aachiwa kwa dhamana
Mchungaji huyo amekuwa mahabusu kwa zaidi ya wiki mbili zilizopita, kufuatia agizo la mahakama la kutaka akamatwe kwa kushindwa kuhudhuria kesi yake, inayohusu tuhuma za kumkashifu Rais Jakaya Kikwete.
Mapema wiki hii, wakili wake aliiomba mahakama impatie dhamana mteja wake.
Uamuzi wa mahakama kukubali ombi hilo , ulifikiwa jana na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, baada ya kiongozi huyo wa DP, kukamilisha masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja,alisaini bondi ya Sh1 milioni.
Pamoja na kutimiza masharti hayo, mchungaji Mtikila pia ametakiwa kusalimisha mahakamani, hati yake ya kusafiria na asitoke nje ya Jiji la Dar es Salaam, bila kibali.
Februari 8, mwaka huu atasomewa maelezo ya awali kuhusu kesi inayomkabili, hatua inayokuja baada ya upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi.
Januari 21, mwaka huu mchungaji Mtikila, kupitia wakili wake Mpale Mpoki, aliwasilisha ombi kwa mahakama kuiomba itengue uamuzi wa kumfutia dhamana.
Hata hivyo wakili wa serikali, Ponsiano Lukosi alilipinga ombi hilo kwa madai kuwa Mahakama ya Kisutu, haina uwezo wa kutengua uamuzi ambao ulikwishautoa.
Lukosi aliiambia mahakama hiyo kuwa kama upande wa utetezi unataka dhamana hiyo itenguliwe, basi inapaswa kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania .
Akimfutia Mtikila katika kesi ya kashfa dhidi ya Rais Kikwete, hakimu Lema alisema mahakama imefikia uamuzi huyo kwa sababu hakuna sababu za msingi zilizokuwa zimetolewa na Mtikila juu ya kushindwa kuhudhuria mahakama.
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Oktoba 21, mwaka jana katika maeneo ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Ilala, jijini Dar es Salaam Mtikila alitoa maneno ya uchochezi na ya dharau na kujenga chuki dhidi ya serikali na Rais.
HABARI HII NI KWA MJIBU WA GAZETI LA MWANANCHI
Post a Comment