Anna Clara Masala: Muziki wa Injili ni kazi ya Mungu, si umaarufu
“Pamoja na ukweli huo lakini nikwambie jambo moja ambalo mimi ninaliona kuwa si sahihi nalo ni ushirikiano mdogo na kukosekana upendo wa dhati miongoni mwetu sisi waimbaji wa muziki wa Injili,” anasema Anna.
Akizungumzia juu ya mwanzo wa huduma yake, Anna anasema kwamba kazi ya uimbaji alianza kuifanya akiwa muimbaji wa kwaya ya kanisani alipokuwa anaabudu, (Tanzania Assemblies of God -TAG-Kinondoni) ambapo kupitia muziki huo, Mungu ameweza kumsimamia kwenye masuala mengi ya kimaendeleo.
Miongoni mwa mambo ambayo anaamini kuwa yametokana na matunda ya kufanya kazi ya kuhubiri Injili kwa njia ya nyimbo, ni pamoja na kupata kazi za kucheza filamu tatu ambazo ni Hero of Church, Kiapo na Danger Zone jambo analoamini kuwa ni kutokana na rehema za Mungu tu.
“Haya kwangu nayaona kuwa ni mafanikio makubwa, lakini haikuwa ni safari nyepesi kwa sababu nilikutana na vikwazo vingi katika maisha yangu, hii si mimi pekee bali waimbaji wengi hukabiliana na mambo haya.
“Pamoja na hayo, pia muziki huu umekuwa ukitumika kwa ajili ya kubadilisha tabia na miondoko ya wanajamii na kumtangaza Mungu, lakini cha kushangaza wapo baadhi ya waimbaji hawapendani, jambo ambalo ni baya kwa mustakabali wa huduma hii,” anaongeza muimbaji huyo ambaye bado hajapata jina kubwa ikilingansihwa na waimbaji wengine waliopo juu hivi sasa kama Rose Mhando, Bahati Bukuku na Upendo Nkone.
Akielezea ushirikiano uliokuwepo baina ya waimbaji chipukizi, anasema kuwa kila wakati wamekuwa wakipeana moyo na kuamini kuwa kufanya muziki wa Injili si kwa ajili ya kutafuta fedha, au umaarufu bali ni kazi ya wito ili kuwaokoa watu wa Mungu na matatizo ya kidunia.
“Japokuwa ni kazi ya Mungu lakini kuna tatizo lingine kubwa nalo ni usumbufu kwenye studio wakati tukijiandaa kurekodi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba studio hizihizi ndizo zinazotumika kurekodi nyimbo za kidunia,” anaongeza mwanadada huyo aliyejikita vilivyo kwenye imani ya kilolole.
Aneleza kuwa studio nyingi za kidunia zinakuwa na matatizo ya kuiba kazi za waimbaji na kuziuza kinyemela huku akikiri kuwa hata yeye alitokewa na jambo hilo .
“Nimalizie kwa kusema kuwa huduma ya uimbaji wa nyimbo za Injili inagusa zaidi kumtumikia Mungu na siyo kujulikana kama baadhi ya watu wanavyodhani, na wakati huo huo niwape moyo watumishi wa Mungu kutokana na kujituma kwao kwenye huduma hii,” anamaliza Anna.
One Response to “Anna Clara Masala: Muziki wa Injili ni kazi ya Mungu, si umaarufu”
Watu wengi wanachanganya kuokoka na kuimba nyimbo za Injili. Inatakiwa unachokiimba kiendane na matendo yako. Nakufahamu vizuri huna ulokole wa aina yoyote, badilika na mungu atakusaidia.
Post a Comment