JICHO LA MUZIKI WA INJILI
Waimbaji wengi wa muziki wa Injili watatupwa motoni
NI siku nyingine imempendeza Mungu tukutane katika safu hii mpya itakayokuwa inazungumzia masuala ya muziki wa Injili ikienda kwa jina la ‘Jicho la Muziki wa Injili’. (Kabula akiwa na Mchungaji Anna Suguye wakiwa kanisani)Nimeamua kuwa naandika masuala haya ili kuwaponya watumishi wengi wa Mungu ambao shetani amekamata ufahamu wao na kujikuta wanafanya dhambi bila wao kujijua. Leo hii baadhi ya waimbaji wa nyimbo za Injili wanaimba nyimbo zenye ujumbe mzito wa kumtukuza Mungu huku wakifanya mambo ambayo hayaendani na wanachokihubiri kwa njia hiyo ya uimbaji.
Yawezekana wewe unaweza ukawa shahidi wa hili ninalolizungumza leo katika safu hii. Hakuna asiyetambua kwamba muziki wa Injili kwa kiasi kikubwa umekuwa ukiwasaidia watu wengi walio kwenye dimbwi la kufanya maovu kuachana na tabia hiyo na kumrudia Muumba wao kwa kuokoka kutokana na maneno mazito na yenye ushawishi ambayo hutumiwa na muimbaji binafsi, kwaya ama kikundi.
Kitu cha kusikitisha katika hili ni kwamba, baadhi ya waimbaji wa muziki huo wameonekana kama kibao cha matangazo kinachomwelekeza mtu kwenda sehemu anayotaka kwenda kama haijui. Matangazo ama mabango mengi ya namna hiyo yamefanyika msaada mkubwa kwa kuwafikisha watu sehemu husika bila usumbufu huku menyewe yakibaki hapo mpaka wakati mwingine yanaota kutu.
Mbali na kuonekana kutoa msaada mkubwa kwa wahusika lakini bango mwisho wa siku hung’olewa na kwenda kutupwa jalalani baada ya kuchakaa na kuonekana uchafu sehemu husika. Leo hii baadhi ya waimbaji wa muziki wa Injili wamekuwa kama mabango ya kuelekeza watu kuachana na maovu na mwisho wa siku kufika salama kwa Muumba wao huku wao wakibaki palepale.
Waimbaji hao asilimia kubwa wamekuwa wakifanya usanii wakati wa kuimba madhabahuni kwa kuonekana wanaimba katika roho na kweli mpaka watu wanabarikiwa kutokana na kuimba kwa ustadi wa hali ya juu na sauti zilizopangiliwa vema.
Kama unafikiri nakudanganya, jaribu kuchunguza kwa umakini, waimbaji wengi leo hii ni waasherati wakubwa, tena wanachukuana wao kwa wao ndani ya kwaya na vikundi vyao. Utakuta wanakwaya wanafanya uchafu huo kwa siri kubwa na hao hao wanasimama kwenye madhabahu kuimba nyimbo za kukemea kuachana na maovu pasipo kuangalia kibanzi kilicho ndani ya macho yao.
Ukifanikiwa kusikiliza nyimbo zao radioni ama kwenye luninga kwa waliofanikiwa kurekodi, utawaona wanaimba kwa kuhisia kali kana kwamba hata leo Masihi akiwachukua wanaenda moja kwa moja peponi, lakini ukweli ni kwamba huo ni usanii pekee na siku ya mwisho nafikiri ndiyo watakuwa wa kwanza kutupwa motoni.
Mimi sielewi ni Mungu yupi wanaomtumika waimbaji wenye tabia hiyo chafu, kwa maana mbali na kufanya uasherati, watumishi hao hao ndiyo walevi, wasengenyaji, wadokozi, wambeya na wenye maneno machafu kinywani mwao.
Inauma sana unaposikia baadhi ya waimbaji wanaenda kwa waganga wa kienyeji kwa lengo la kusafisha nyota zao ili nyimbo zao zipate kibali machoni mwa Watanzania na hata nje ya nchi. Bila aibu baadhi yao huwa wanafukiza dawa kabla ya kupanda madhabahuni ili anatakapopewa nafasi kuimba kila mmoja amfurahie na ikiwa pamoja na kutuzwa fedha kutokana na uimbaji mzuri.
Sasa unaweza kujiuliza swali: Je, inakuwaje watu hawa wanatenda maovu na wanaimba kwa upako lakini Mungu bado amewaruhusu kufanya hivyo? Jibu ni kwamba kipindi hiki ni cha neema, Mungu anakuwa kama hawaoni, lakini ukweli ni kwamba ipo siku atakuja kuwafedhehesha saa na majira wasiyoyajua.
Kinachowaponza waimbaji wengi ni kitendo cha kuathiliwa na tabia zao walizokuwa nazo kabla ya kuokoka, hivyo wasiposimama imara hujikuta wanarudi walikotoka huku wakiona wanachokifanya ni sasa.
Ieleweke kuwa kuokoka ni rahisi lakini kuutunza wokovu ni kazi kubwa, ndiyo maana waimbaji hao ambao huokoka baada ya kupanda neno la Mungu mioyoni, wasiposimama imara hujikuta wanarudi nyuma kutokana na kukumbuka walikotoka.
Post a Comment