ERIC SHIGONGO ATOA WARAKA WA UCHAGUZI
Ndugu zangu,
Watanzania wenzangu,
Tumsifu Yesu Kristo,
Bwana Yesu asifiwe,
Asalam Aleykhum,
Katiba yetu ya Jamhuri ya Tanzania inatutaka kila baada ya miaka mitano tufanye uchaguzi wa viongozi wetu watakaotuongoza kwenda kwenye nchi ya ahadi kwa miaka mitano, tangu uhuru wetu tumekuwa tukilifanya jambo hili na kujipatia viongozi ambao hakika wametufikisha hapa tulipo.
Kwa mara nyingine tena jambo hili linatokea kesho kutwa (Jumapili), Watanzania tunashiriki katika zoezi hili la kuchagua Rais na Wabunge wetu watakaotuongoza kwa miaka mitano ijayo. Nyote mtakubaliana nami kuwa katika historia ya nchi yetu hapajapata kuwepo na uchaguzi wenye ushindani na changamoto kali kama ilivyotokea katika uchaguzi huu wa mwaka 2010, tangu katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) tumeshuhudia ushindani mkali kati ya wagombea kuliko uchaguzi mwingine wowote uliowahi kufanyika nchini mwetu. Hili ni jambo la kujivunia.
Keshokutwa ni siku muhimu sana katika maisha yetu, siku ambayo tutafanya maamuzi juu ya maisha yetu ya baadaye kwetu sisi na watoto wetu ambao hawatashiriki kupiga kura, hii ina maana tumebeba dhamana kubwa sana ya watoto na wajukuu zetu pia, keshokutwa ndio siku ambayo sisi Wananchi wa kawaida tutaonyesha uwezo wetu kwamba ndio waajiri wa viongozi wetu. Hakika hii ni siku muhimu sana .
Nimeamua kuandika waraka huu kwa lengo la kuwakumbusha jambo moja kwamba, kwa miaka 49 tangu tupate uhuru, nchi yetu imefaidi amani na utulivu ambao majirani zetu wengi hawana. Amani ni kitu adimu sana nchini Kenya, Uganda, Burundi, Sudan na kwingineko, walifanya makosa yaliyofanya Njiwa wa Amani akaruka na kuondoka zake!
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu,
Ni vyema kukumbuka kuwa, katika maamuzi yetu ya keshokutwa, kosa dogo tu linaweza kufanya amani ya nchi hii kuwa historia, jambo ambalo binafsi sitaki kulishuhudia kwa macho yangu na hata vizazi vijavyo sitaki vije kunihukumu kuwa nilishindwa kuitunza Amani. Hakuna anayewaza kwamba kama hatutafanya maamuzi sahihi keshokutwa, tuna masaa machache kabla historia ya nchi yetu haijabadilika kwani hata katika nchi zisizo na amani walianza hivi hivi na hakuna aliyekuwa na taarifa kwamba wangeishia kwenye kambi za wakimbizi.
Watanzania wenzangu,
Nchi yetu imepita katika vipindi vigumu vingi; wakati wa kupigania uhuru wa nchi yetu kutoka kwa Wakoloni, Azimio la Arusha, Operesheni Vijiji, Vita vya Kagera, kuzama kwa MV Bukoba, uchaguzi wa mwaka 2005 n.k., lakini katika vipindi vyote hivi tulisimama pamoja kama nchi, kuhakikisha tunazishinda changamoto hizo tukiwa familia moja ya Watanzania. Ndugu zangu hii ndiyo historia yetu kama Watanzania, ya kupanda pamoja na kushuka pamoja. Kulia pamoja na kufurahia pamoja.
Kwa mara nyingine tena ndugu zangu, keshokutwa asubuhi Busara, Hekima na Uvumilivu wetu unawekwa kwenye mzani ili upimwe, ndio maana naandika waraka huu kabla ya siku ya kesho kuwaasa tuifikirie Tanzania yetu, tuwafikirie watoto wetu, tuwafikirie wajukuu zetu na kujiepusha na maamuzi mabaya yatakayotokana na chuki, jazba na hasira na kuchukua uamuzi utakaokuwa na faida kwetu na vizazi vitavyokuja baada ya sisi.
Kuna vyama vilivyosimamisha wagombea wa Urais na Wabunge, kipo Chama Cha Mapinduzi, CHADEMA, CUF, UDP, TLP, NCCR-Mageuzi, APPT Maendeleo, NLD, Demokrasia Makini, CHAUSTA, UMD, SAU, NRA, AFP, UPDP, JAHAZI Asilia na TADEA. Kati ya vyama vyote hivi hakuna hata kimoja cha kukipuuza, hakuna anayeweza kudai Chama fulani ni bora kuliko kingine, wenye uamuzi huo ni wananchi wa Tanzania hiyo siku ya keshokutwa.
Vyote ni vyama, kila kimoja kinataka kiwe kinara katika safari yetu kuelekea katika nchi ya ahadi na vyote vina wafuasi waliotapakaa nchi nzima na watapiga kura siku ya keshokutwa. Hii ina maana kwa sababu ya tofauti za Kiitikadi, Watanzania tumegawanyika katika makundi, wapo CCM, wapo TLP, wapo CUF n.k.
Ndugu zangu,
Pamoja na tofauti zetu hizi, bado tunaunganishwa na kitu kimoja kikubwa ambacho ni Utanzania wetu, mwisho wa siku sisi ni Watanzania watoto wa baba mmoja atiwaye Tanzania na tunafanana katika jambo moja; HATIMA! Hatima yetu ni moja, hakuna anayeweza kukataa ukweli kwamba sote tunahitaji huduma bora za afya, elimu bora kwa watoto wetu, barabara, maji, ajira na nafasi sawa ya kuendelea mbele kimaisha. Usawa wetu huu, ndio unatufanya tuweke pembeni tofauti zetu zote na kufanya maamuzi sahihi siku ya kesho.
Kila mmoja wetu anayo haki ya kumchagua kiongozi yeyote anayempenda bila kushinikizwa, hii ni haki ya Kikatiba. Waraka huu hauna lengo la kumshawishi mtu yeyote achague Chama fulani na akiache kingine, bali ni kukumbusha Utanzania na Amani yetu, mambo mawili makubwa ambayo hakika hatuhitaji kuyapoteza kwa gharama yoyote kwani kuyarejesha ni kazi ngumu ambayo inaweza hata kugharimu maisha yetu.
Nayasema haya sababu mengi yameongewa na Wanasiasa wakati wa kampeni kwa lengo la kutushawishi tuwaunge mkono, tumeshuhudia hata vifo vya watu sababu ya Siasa! Jambo ambalo hakuna mtu aliyetegemea wakati kampeni zinaanza.
Wapo waliohubiri chuki za kidini majukwaani na hata madhabahuni, wapo waliohubiri Ukabila, rangi na kadhalika ili tu wajipatie wafuasi bila kufahamu kuwa hiyo ni mbegu mbaya ambayo kabla ama baada ya uchaguzi inaweza kuliteketeza Taifa letu na kutuacha baadhi yetu makaburini na Amani ambayo kwa kipindi kirefu tumejivunia ikiwa imepotea. Viongozi wa aina hii siku ya keshokutwa hata kama ni wataalam kiasi gani wa kuongea majukwaani, inabidi wanyimwe kura.
Katika kitabu cha Paulo Coelho, kiitwacho The Alchemist, anaongelewa mchungaji mmoja kijana aitwaye Santiago, ambaye ndoto yake ilikuwa ni kusafiri dunia nzima ambapo aliacha masomo ya Upadri ili awe mchunga Kondoo na kutimiza lengo lake. Katika safari yake aliswaga kundi la Kondoo kuelekea katika nchi ya Andalusia .
Aliwapeleka kondoo alikotaka yeye na kuwafanya wafanye alivyotaka, kama alitaka wanywe maji aliwapeleka bwawani na kama alitaka wale nyasi aliwapeleka malishoni. Siku moja Santiago alisimama na kuwaangalia kondoo wake kwa huruma moyoni mwake akasema: “Hawajui niwapelekako, nikiamua kuwachinja mmoja baada ya mwingine hakuna atakayeshtuka wala kukimbia, kwani hawa ni Kondoo, wa mwisho atajikuta ameshabaki peke yake lakini bado hatakimbia.”
Ndugu zangu,
Siku ya keshokutwa tuna kazi kubwa ya kuchagua wachungaji watakotuchunga kwa miaka mitano, hivyo ni lazima tunahakikisha tunachagua mchungaji ambaye hatatutelekeza kama kondoo wa Santiago, tukatae kufanywa Kondoo bali tufanye maamuzi yenye faida kwetu, badala ya kupelekwa au kuhamasishwa na jazba tunazopandikizwa.
Tukumbuke sisi ndio nguvu ya taifa hili, lazima tuwakatalie watu wote wanaotaka kutugawa na kuiingiza nchi yetu katika matatizo eti kwa sababu tu wanataka kwenda Ikulu. Tusiwe kondoo bali tuwe na uwezo wa kuchanganua kila sentensi inayotoka midomoni mwa Wanasiasa, tukikumbuka msemo usemao “Nyuma ya sentensi ya mwanasiasa kuna sentensi nyingine.” Wanasiasa walio wengi huwa hawamaanishi wanachokisema, siku zote wana moja kichwani.
Hivyo ni vizuri kuachana na sentensi za mbele na kwenda nyuma ya sentensi hizo, huko ndiko tutaukuta ukweli kuwa lengo halikuwa kusomesha watu bure au kuondoa kodi, au kutimiza ahadi zote zinazotolewa bali ni Ikulu vichwani mwao! Kwa akili alizotupatia Muumba wetu ni lazima tuwe na uwezo wa kupambanua kila jambo na kufanya uamuzi sahihi siku ya kesho.
Uamuzi wowote utakaofanya, usiwe wa ushabiki tu bali utakaotuwezesha kusonga mbele kama nchi moja, watu wamoja na baada ya uchaguzi, sote tukubaliane na matokeo kama CCM watakuwa wameshindwa wawe tayari kuwaachia Wapinzani ili haki itendeke na kama Chadema au CUF au TLP watakuwa wameshindwa kwa haki asiwepo mtu yeyote wa kukataa matokeo na kutushauri sisi Watanzania tuingie mitaani na kufanya vurugu ambazo mwisho wa siku zitaiondoa Amani yetu.
Najua vijana wengi wamejazwa jazba kwamba kama matokeo hayatakuwa kama walivyotaka wao basi damu itamwagika, lakini niseme jambo moja kwamba ni mtu mjinga tu anaweza kukubaliana na jambo hili na kutumiwa kama ngazi na Wanasiasa na hatimaye kutesa ndugu zake. Ukishindwa kubali, baada ya hapo tuungane kujenga Majimbo na nchi yetu.
Ndugu zangu,
Hakuna kitu kibaya kama kupoteza amani, angalieni majirani zetu wanavyoihangaikia! Ni vizuri sana kujifunza kutoka kwao kabla sisi hatujafikiria kujiingiza katika vurugu sababu ya wanasiasa ambao siku zote wapo tayari kuingia Ikulu hata kama gharama ni damu yetu! Hii sio sahihi hata kidogo, lazima tuzikatae kauli hizi kutoka kwa wanasiasa na keshokutwa tufanye maamuzi sahihi yenye manufaa kwa nchi yetu.
Chama tawala (CCM) kimejieleza kupitia kwa Mgombea wake, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kimejinadi kwamba pamoja na matatizo yanayosababishwa na umasikini, kimejitahidi kadri ya uwezo wake kujenga Uchumi wetu. Vyama vya Upinzani navyo viliendelea kudai hakuna kilichofanywa na CCM tangu Uhuru wetu, yote ni mabaya! Yote ni sifuri! Sana sana ni ufisadi peke yake! Hivyo wachaguliwe wao ambao wataboresha maisha ya Watanzania.
Wakati mwingine tumesikia hata Matusi katika majukwaa ya Kisiasa zote hizi ni kampeni lengo ni kuitafuta kura yangu na yako. Ndugu yangu, sitaki kukushawishi keshokutwa umchague fulani, ila nasema tumia akili yako kama mzani ili upime kauli za Wanasiasa na kuona kama tunakwenda mbele au tunarudi nyuma kama nchi, Mgombea mwongo yeyote hastahili kupewa kura yako.
Nchi yetu iko njia panda, inahitaji viongozi imara wanaoweza kuchagua kwenda kulia ama kushoto si kubaki katikati, kama kweli tunahitaji kusonga mbele. Binafsi sikubaliani na nafasi ya pili ama ya tatu katika Afrika Mashariki, lazima siku moja Tanzania iwe namba moja. Jambo hili linawezekana kama tutaweka uongozi imara madarakani.
Hata kama hali ni ngumu kiasi gani ni lazima tuchukue hatua makini kusogea mbele! Huu ni ukweli. Najua kama Watanzania tunayo matatizo mengi hivyo kiongozi yeyote tutakayemchagua kesho lazima awe ni yule atakayetuhakikishia kwamba atashughulikia matatizo yetu si tu hotuba nzuri jukwaani na jazba nyingi zisizo na kipimo.
Siku ya keshokutwa ndio siku ya kufanya uamuzi huu muhimu bila kufanya makosa, tuwapime wagombea wetu kwa historia zao na mafanikio waliyotuletea katika nyanja nilizozitaja hapo juu!
Siku ya keshokutwa ni siku ambayo tunatakiwa kufanya si tu mambo yanayoshangiliwa na wengi bali mambo ya lazima kufanya, hata kama hayatashangiliwa ili mradi yawe na faida kwa nchi yetu. Kwa haya niliyoyasema ndugu zangu nawaomba siku ya keshokutwa tuwe makini sana katika uamuzi tutakaofanya, kamwe tusifuate ushabiki tu na kuwa bendera inayofuata upepo, bali tutumie akili zetu vizuri kuchagua viongozi bora watakaotuvusha kipindi cha miaka mitano kwa mafanikio. Kwa haya machache nawatakieni uchaguzi mwema siku ya kesho, utakapoingia kwenye chumba cha kupigia kura, ifikirie nchi yetu, fikiria wazazi wako, watoto wako, ndugu zako, rafiki zako baada ya hapo Mungu akusaidie ufanye uamuzi sahihi.
Mungu ibariki Tanzania ,
Mungu wabariki Watanzania.
Ahsanteni.
One Response to “ERIC SHIGONGO ATOA WARAKA WA UCHAGUZI”
Najua comment hii haitatoka kwani itakufanya UFUKUZWE KAZI lakini naandika tu anyway.
Mwambie Shigongo kwamba mimi nataka ZE UTAMU irudi. Mbona alitishwa tu kidogo halafu akaiua??? Mwoga nini?
Please soma huu mjadala hapa:
http://changamotoyetu.blogspot.com/2010/09/mimi-najifunza-kitu-wewe-je.html
Kalagabaho na shigongo wako.
Post a Comment